Dar es Salaam, Oktoba 15, 2025: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameungana na taifa la Kenya kuomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Amolo Odinga, aliyefariki dunia leo nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia amesema amepokea taarifa za kifo cha Odinga kwa masikitiko makubwa, akimtaja kama kiongozi mahiri, mpenda amani na mtafuta suluhu ambaye mchango wake haukuishia Kenya pekee bali ulienea Afrika Mashariki na bara lote la Afrika.
“Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote,” alisema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa Odinga alikuwa Mwanamajumui wa kweli, mwenye ushawishi mkubwa na aliyeheshimika kwa ujasiri wake katika kutetea haki, demokrasia na mshikamano wa kijamii.
Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, Rais Samia ametuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, mjane wa marehemu Mama Ida Odinga, familia, ndugu, jamaa na wananchi wote wa Kenya.
“Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki kigumu, na ailaze roho ya mpendwa wetu Mheshimiwa Raila Amolo Odinga mahali pema peponi. Amina,” alisema Rais Samia.
Kifo cha Raila kimeibua simanzi kubwa kote Afrika Mashariki, ambapo viongozi na wananchi wameendelea kutoa salamu za rambirambi wakimtaja kama nguzo muhimu ya siasa na mshikamano wa kikanda.



Toa Maoni Yako:
0 comments: