Rais wa Kenya, William Ruto, ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani na kiongozi wa ODM, Raila Amolo Odinga.
Akihutubia taifa kupitia televisheni jana jioni, Rais Ruto alimtaja marehemu Raila kama “mzalendo mwenye ujasiri usio wa kawaida” ambaye alitumia maisha yake yote kutetea demokrasia, haki na mshikamano wa taifa.
Katika kipindi hiki cha maombolezo, Rais Ruto amesema bendera ya taifa zitapepea nusu mlingoti katika maeneo yote ya umma nchini Kenya na katika balozi zote za Kenya nje ya nchi.
“Kama ishara ya heshima, nimeahirisha shughuli zangu zote za umma kwa siku zijazo, na ninawaomba wafanyikazi wote wa umma pamoja na viongozi wengine kufanya vivyo hivyo ili tuungane kama taifa katika maombolezo haya,” alisema Rais Ruto.
Aidha, Rais Ruto ametangaza kuwa serikali itampatia Raila Odinga mazishi ya kitaifa yenye heshima kamili, kama inavyostahili kiongozi wa kitaifa.
Serikali ya India, ambako Raila alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu, imeahidi kushirikiana na Kenya kuhakikisha mwili wa kiongozi huyo unarejeshwa nyumbani kwa heshima zote.
Ujumbe maalum unaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi, pamoja na mke wa marehemu, Mama Ida Odinga, unatarajiwa kusafiri kwenda India kusimamia taratibu za mwisho za kuurejesha mwili wake nchini.
Kifo cha Raila Odinga kimeibua simanzi kubwa ndani na nje ya Kenya, huku viongozi wa kitaifa, wa kimataifa, na wananchi wa kawaida wakiendelea kuomboleza kuondokewa na kiongozi ambaye alikuwa kiungo muhimu katika siasa na historia ya taifa hilo.



Toa Maoni Yako:
0 comments: