Nairobi, Jumatano: Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na Kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Amolo Odinga, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.
Taarifa zinaeleza kuwa Odinga alifariki Jumatano hii wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja nchini India, baada ya siku kadhaa za kuwepo kwa taarifa zilizodai kuwa hali yake ya kiafya ilikuwa tete.
Kabla ya kifo chake, familia yake na viongozi wa karibu walikuwa wametupilia mbali taarifa hizo, wakisisitiza kuwa kiongozi huyo alikuwa mzima na akiendelea kupata nafuu.
Seneta wa Siaya na kaka mkubwa wa Raila, Oburu Odinga, alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa tetesi za kwamba kiongozi huyo alikuwa katika hali mbaya zilikuwa za kupotosha.
“Natamani kuwaambia Wakenya kwamba Raila anaendelea vizuri. Kama binadamu mwingine yeyote, aliugua kidogo lakini sasa anapumzika na kupata nafuu,” alisema Oburu.
Aliongeza kuwa hali ya kiongozi huyo haikuwa kama ilivyodaiwa na vyombo vya habari, na akawataka wananchi watulie wakisubiri kumwona akirejea.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Naibu Rais Kithure Kindiki pamoja na rafiki wa muda mrefu wa Raila, ambaye pia ni mfanyabiashara na mmiliki wa vyombo vya habari, S.K. Macharia.
“Waziri Mkuu yuko salama na mwenye afya. Nimezungumza naye, na wale wanaomtakia mabaya hawana nia njema. Si mila ya Kiafrika kumtakia mtu mabaya,” alisema Kindiki.
Naye Macharia aliongeza: “Asubuhi ya leo nimezungumza naye, na jana pia nilimpigia simu. Raila yuko mwenye afya nzuri, na baada ya siku chache atakuwa nasi tena.”
Kifo cha Raila Odinga kinahitimisha safari ndefu ya kisiasa iliyojaa changamoto na mafanikio, akiwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri na wenye ushawishi mkubwa zaidi katika historia ya Kenya na Afrika Mashariki.



Toa Maoni Yako:
0 comments: