Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 10,763.94 za dawa za kulevya aina mbalimbali pamoja na kilogramu 6,007 na lita 153 za kemikali bashirifu, huku watuhumiwa 89 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 21, 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mafanikio hayo yametokana na operesheni zilizofanyika Septemba na Oktoba katika maeneo mbalimbali nchini.

Lyimo alieleza kuwa katika operesheni ya Kariakoo, Dar es Salaam, mamlaka ilikamata dawa aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 40.32, zilizokuwa zimekaushwa na kufungwa kama viungo kwenye paketi 80 zenye maandishi “Dry Basil Leaves”. Dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kwenda Canada na Italy kupitia makampuni ya usafirishaji.

Waliohusishwa na tukio hilo ni Yusuphu S. Kibaha (35) na Mohamed H. Ramadhan (41), ambapo uchunguzi umebaini dawa hizo ziliingizwa nchini kwa njia za kificho kutoka nchi jirani.

“Mtandao huu wa usafirishaji wa mirungi unatumia bodaboda na baadhi ya mawakala wa kampuni za usafirishaji. Hatutalifumbia macho jambo hili, kwani linaweza kuathiri taswira ya nchi kimataifa,” alisema Lyimo.
Katika tukio jingine Mlalakuwa, Kinondoni, DCEA iliwakamata vijana wanne wakitengeneza biskuti za bangi kwa ajili ya “house party” ya wanafunzi wa vyuo vikuu. Watuhumiwa hao ni Bright Malisa, Humphrey Safari, Novatus Kileo na Chriss Mandoza, wote wenye umri wa miaka 26.

Walikutwa na biskuti 140 za bangi, puli nane na paketi tisa za bangi zenye jumla ya kilo 2.858.

“Hii inaonesha namna vijana wanavyohatarisha maisha yao kwa kutumia dawa za kulevya kama sehemu ya starehe,” alisema Lyimo.

Kamishna Jenerali huyo pia alisema uchunguzi unaendelea kubaini matumizi ya bangi kwenye bidhaa mbalimbali kama vinywaji, vyakula, vipodozi na sigara za kielektroniki (vapes), ambazo baadhi zimegundulika kuwa na viambata vya bangi.

Katika operesheni mikoani, DCEA ilikamata bangi kilo 9,164.92, mirungi kilo 1,555.46, skanka gramu 367 na heroin gramu 7.498, pamoja na kuteketeza ekari 11.5 za mashamba ya bangi.

Lyimo alitoa onyo kali kwa bodaboda, wamiliki wa kampuni na mawakala wa usafirishaji kuwa makini na mizigo wanayosafirisha, na pia aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kuepuka matumizi ya dawa za kulevya.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: