Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Viongozi wa jamii ya Kimasai nchini Tanzania, maarufu kama Malaigwanani, wametoa tamko lao rasmi la kulaani vikali watu wanaohamasisha maandamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa.
Tamko hilo lilitolewa katika eneo la Donyomorwak, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, wakati wa mkutano wa kawaida wa Orkiama, ambapo Katibu wa Malaigwanani Tanzania, Jeremia Laizer, alisoma tamko hilo kwa niaba ya viongozi wa jamii hiyo.
“Tunawahimiza wananchi wote kudumisha amani, mshikamano na utulivu kuanzia ngazi ya shina hadi taifa zima. Tukatae uchochezi, migawanyiko na fitina. Tuchague maendeleo, umoja na mustakabali mwema wa vizazi vijavyo. Tanzania kwanza, amani kwanza,” alisema Bw. Laizer.
Aliongeza kuwa Malaigwanani wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kulinda amani na ustawi wa taifa, huku wakihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa utulivu na heshima siku ya uchaguzi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Namelok Sokoine, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwapongeza Malaigwanani kwa kuonesha uzalendo na hekima katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Jamii hii imekuwa mfano wa kuigwa kwa kuunga mkono juhudi za kulinda amani na utulivu wa nchi. Wananchi wote wajitokeze kupiga kura bila hofu wala uchochezi,” alisema Sokoine.
Viongozi wengine wa jamii hiyo waliahidi kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao, wakionya kuwa maandamano yasiyofuata taratibu mara zote huishia katika uharibifu wa mali na kuvuruga amani, jambo linalowaathiri zaidi wanawake, watoto na wazee.
Mkutano huo ulisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila Mtanzania, huku ujumbe wa pamoja wa Malaigwanani ukiwa: “Tanzania kwanza, amani kwanza.”








Toa Maoni Yako:
0 comments: