BLANTYRE, Malawi — Historia imejirudia nchini Malawi baada ya Tume ya Uchaguzi (MEC) kutangaza rasmi jana kwamba Peter Mutharika, aliyewahi kuiongoza nchi hiyo, ameshinda uchaguzi wa urais kwa kishindo kikubwa na kurejea tena madarakani.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa, Mutharika amejinyakulia zaidi ya 56% ya kura halali, huku mpinzani wake mkuu na Rais aliyemaliza muda wake, Lazarus Chakwera, akipata takribani 33% pekee. Hii ni mara ya pili kwa Mutharika kurejea Ikulu baada ya kupoteza kiti hicho mwaka 2020 kufuatia hukumu ya Mahakama ya Katiba iliyofuta matokeo ya awali kutokana na dosari kubwa za uchaguzi.
Katika hotuba yake ya kitaifa, muda mfupi kabla hata ya matokeo rasmi kutangazwa, Rais Chakwera alionesha ukomavu wa kisiasa kwa kukubali matokeo na kumpongeza mpinzani wake.
“Kwa heshima ya wananchi na katiba, nakiri kuwa ndugu yangu Peter Mutharika anaongoza kwa kishindo. Nampongeza kwa ushindi huu na ninawaomba wananchi wote kudumisha amani,” alisema.
Safari ya Mutharika kurejea madarakani
Mutharika, mwanasiasa mkongwe na profesa wa sheria, alitawala Malawi kuanzia mwaka 2014 hadi 2020. Kuondolewa kwake madarakani kulitokana na kashfa ya “tippex election”, ambapo Mahakama ya Katiba ilifuta matokeo kwa madai ya udanganyifu mkubwa. Lakini sasa, miaka mitano baadaye, amerejea tena kwa kishindo kupitia sanduku la kura, akiahidi kurejesha nidhamu ya kifedha na kupambana na hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi.
Uchaguzi ulivyokuwa
Zaidi ya wapiga kura milioni 9 walijiandikisha kushiriki uchaguzi huu, ambao umeelezewa na waangalizi wa kimataifa kuwa wa amani na huru, licha ya changamoto ndogo katika baadhi ya vituo. Uhamasishaji mkubwa wa wananchi ulitokana na hali mbaya ya kiuchumi — mfumuko wa bei, uhaba wa chakula na mafuta, pamoja na athari za ukame na dhoruba — mambo yaliyosababisha hasira dhidi ya serikali ya Chakwera.
Sauti za wananchi na matarajio mapya
Baadhi ya wananchi waliozungumza na vyombo vya habari walieleza matumaini yao mapya chini ya uongozi wa Mutharika.
“Tunataka maisha bora, bei ya chakula ishuke, na ajira zipatikane. Tunaamini Mutharika atatupa matumaini mapya,” alisema mmoja wa wakazi wa Lilongwe.
Waangalizi pia wameitaka serikali mpya kuhakikisha inaimarisha taasisi za kidemokrasia, ikiwemo Tume ya Uchaguzi, ili kuepuka marudio ya migogoro ya kisiasa kama ilivyotokea mwaka 2019.
Changamoto zinazomsubiri
Licha ya ushindi wake, Mutharika anakabidhiwa taifa lililojaa changamoto. Uchumi umedorora, mfumuko wa bei unakandamiza wananchi, na huduma za kijamii kama afya na elimu zinahitaji mageuzi makubwa. Zaidi ya hapo, Malawi inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazochochea njaa na umasikini.
Kwa ushindi huu, Peter Mutharika anajiandaa kuapishwa na kurejea Ikulu ya Lilongwe, akibeba matarajio makubwa ya wananchi waliompa ridhaa ya pili. Wakati huo huo, kitendo cha Chakwera kukubali matokeo mapema kimepongezwa ndani na nje ya Malawi, kikichukuliwa kama mfano wa kuigwa wa demokrasia barani Afrika.




Toa Maoni Yako:
0 comments: