Na Mwandishi Wetu, Chakechake – Pemba

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi wa Pemba kuwa Serikali itaendelea kusimamia usawa wa miradi ya maendeleo kati ya Unguja na Pemba.

Akizungumza Septemba 24, 2025 na wafanyabiashara na wajasiriamali wa soko la Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba, Dkt. Mwinyi alisema katika miaka mitano iliyopita Serikali yake imewekeza katika sekta muhimu ikiwemo miundombinu, elimu na afya kwa uwiano unaozingatia pande zote mbili za visiwa.

Kuhusu sekta ya biashara, Dkt. Mwinyi aliahidi kulilinda na kuliendeleza soko la asili la Chakechake kwa kulibakisha katika uasili wake, sambamba na mpango wa kujenga soko jipya la kisasa litakalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara na wananchi.

Katika kuimarisha uchumi wa wananchi, alieleza kuwa awamu ijayo ya Serikali itaongeza mara dufu fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi, ili kila mjasiriamali aweze kufikiwa na mikopo bila kubaki nyuma.

Aidha, aligusia malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu wingi wa kodi, akibainisha kuwa Serikali itafanya mapitio ya kina na kuweka utaratibu wa kodi nafuu, ili kutoa unafuu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

“Serikali imedhamiria kuongeza fursa za maendeleo kwa kila mmoja wenu. Nawaomba mniruhusu kwa kura zenu ili niendelee kusimamia miradi hii kwa manufaa ya wananchi wote wa Pemba na Unguja,” alisema Dkt. Mwinyi huku akishangiliwa na wananchi.

Katika ziara hiyo, alitoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wote wa Pemba kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuichagua CCM ili iendelee kusimamia maendeleo ya Zanzibar.









Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: