Na Mwandishi Wetu, Unguja
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amehutubia maelfu ya wananchi wa Mjini Unguja huku akiendelea na kampeni za kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza amani na utulivu kama nguzo muhimu ya taifa.
Akizungumza leo, Septemba 17, 2025, katika uwanja wa Kajengwa, Jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini, mkoani Kusini Unguja, Dk. Samia alisema utulivu wa kisiasa ni msingi wa maendeleo na ustawi wa Watanzania wote.
“Tunaingia kipindi cha uchaguzi. Ahadi kubwa niliyotoa nilipoanza ni kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi yenye amani na utulivu. Nilipotembelea Pemba, wazee waliniongoza kunisisitizia kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu, na hili ndilo nalotaka kulipa kipaumbele,” alisema Dk. Samia.
Alibainisha kuwa uchaguzi siyo vita bali ni tendo la kidemokrasia, ambapo wananchi wanatakiwa kwenda kupiga kura kwa utaratibu uliowekwa na kurejea nyumbani ili nchi ibaki salama.
“Siyo kila mara kushika silaha kunaweza kuleta suluhisho. Amani na utulivu wa nchi ni jambo la msingi zaidi kuliko mengine. Niwaombe sana Watanzania kudumisha hali hiyo,” alisisitiza.
Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na vya Zanzibar vimejipanga kikamilifu kulinda amani na usalama wa taifa wakati wote wa uchaguzi.
“Hutaki kishindo, kapige kura kisha rudi nyumbani utulie. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko imara kuhakikisha nchi inabaki salama,” aliongeza.
Mbali na kuhimiza amani, Dk. Samia alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Unguja kumpa kura yeye na wagombea wa CCM katika nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani, ili chama hicho kiendelee kuongoza juhudi za maendeleo nchini.











Toa Maoni Yako:
0 comments: