Na Oscar Assenga, TANGA

Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Tanga imemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua mbalimbali za kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili wafanyabiashara na kuweka mazingira bora ya kufanya biashara.

Akizungumza jijini Tanga, Katibu wa JWT mkoa huo, Ismail Masoud, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeondoa vikwazo vingi, hatua iliyochangia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Alitaja miongoni mwa changamoto zilizotatuliwa kuwa ni upatikanaji wa umeme, ambapo tatizo hilo limepungua kutokana na kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere, na pia ucheleweshaji wa mizigo bandarini, ambapo sasa huduma zinatolewa kwa ufanisi.

“TRA imeboresha mfumo wa ulipaji kodi, wafanyabiashara tunalipa kodi kwa hiari na kwa wakati, jambo lililopelekea malengo ya makusanyo kuzidiwa. Hii ni ishara ya ushirikiano bora kati ya Serikali na wafanyabiashara,” alisema Masoud, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya JWT.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa JWT Mkoa wa Tanga, Fredy Mmasy, alisema utulivu wa biashara nchini umechochea makusanyo makubwa ya kodi, ambayo yamewezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama barabara, hospitali, shule na ununuzi wa magari ya wagonjwa.
Aidha, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Thomas Masese, alithibitisha kuongezeka kwa makusanyo, akieleza kuwa mwaka 2024/2025 walikusanya shilingi bilioni 330 kati ya lengo la bilioni 335, sawa na asilimia 98 ya ufanisi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 61 ukilinganisha na mwaka uliotangulia.

Masese aliongeza kuwa kwa mwaka huu wametengewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 361 na ana imani litafikiwa kutokana na ushirikiano mzuri na wafanyabiashara.
Wafanyabiashara wengine akiwemo Pateli wa Jiji la Tanga na Alphonce Mboya, mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na umeme, waliipongeza Serikali kwa kuondoa vikwazo ikiwemo malipo ya madeni ya nyuma na kupunguza tozo ya hotel levy kutoka asilimia 10 hadi 2.

“Hatua hizi zimeonyesha wazi namna Rais Samia anavyowajali wafanyabiashara na kutupa mazingira ya kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya Taifa,” walisema.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: