Na Mwandishi Wetu.

MGOMBEA wa nafasi ya udiwani Kata ya Makurumla, Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bakari Kimwanga, amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano na wananchi kukamilisha miradi ya maendeleo.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo leo, Agosti 19, 2025, Kimwanga alisema wananchi wa Makurumla wana kiu ya kasi ya maendeleo, hivyo ataendeleza kazi iliyofanyika kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Katika uchaguzi wa mwaka 2020 hadi 2025 tuliahidi na tumetekeleza kwa kushirikiana na wananchi. Sasa tunakwenda hatua ya pili, mwaka 2025 hadi 2030, kukamilisha miradi tuliyoianzisha,” alisema Kimwanga.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuiamini CCM kwa kumpa kura za ushindi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge wa Ubungo na diwani wa Makurumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Makurumla, Idd Toatoa, alisema wanachama wamejitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wao, ishara kuwa chama kiko imara kuelekea uchaguzi.

“Wanachama wameonyesha hamasa kubwa. Tutaendelea kushirikiana kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa mgombea wa Urais, Ubunge na Udiwani,” alisema Toatoa.

Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Kata ya Makurumla, Abdallah Mnyuka, alisema mwaka 2020 kata hiyo iliweka rekodi ya kutoa kura nyingi zaidi kwa wagombea wa CCM, na mwaka huu wanatarajia kuvunja rekodi hiyo kwa kuipa CCM ushindi mkubwa zaidi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: