Na Mwandishi Wetu.
Joshua Adam Kayombo maarufu kama JOKA, amethibitisha nia yake ya kugombea nafasi ya Ujumbe katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
Kayombo, ambaye ni Mpimaji Njia na Msimamizi wa Mbio aliyethibitishwa Kimataifa kwa kiwango cha Grade C, amekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya mbio na riadha nchini. Kwa miaka kadhaa amebahatika kupima na kusimamia njia za mashindano mbalimbali makubwa ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo:
● CRDB International Marathon
● NBC Dodoma Marathon
● Run for Autism
● Zanzibar International Marathon
● Women’s Run
● Hedhi Salama Marathon
● Run for Insight
● Utu Kwanza
● MOI Marathon
● GBV Prevention Marathon
Mbali na hayo, Kayombo pia amehitimu mafunzo ya usimamizi wa michezo ya vikwazo (OCR Level 1), jambo linalompa sifa ya kipekee miongoni mwa wadau wa riadha.
Akizungumza baada ya kuthibitisha nia yake, Kayombo alisema anaingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha riadha nchini kupitia taaluma, nidhamu na ubunifu.
“Nataka kutumia uzoefu wangu wa kimataifa na ndani ya nchi kuboresha riadha, hasa kwenye maeneo ya maandalizi ya mbio, usimamizi wa mashindano na kuendeleza vipaji vipya, ili kupata wachezaji wengi wa kimataifa kwa kupata mbio zenye ubora wa kimaifa” alisema JOKA.
Wadau wa michezo wamempokea vyema Kayombo wakimwelezea kama kiongozi kijana mwenye maono, uthubutu na uzoefu unaohitajika katika kusukuma mbele riadha ya Tanzania.
Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) unatarajiwa kufanyika leo Agosti 16, 2025 na unaleta matumaini mapya kwa wadau wa michezo hususan riadha.







Toa Maoni Yako:
0 comments: