Na Mwandishi Wetu.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) inaendelea kuunda Mfumo wa Jamii X-Change ambao ukikamilika utakuwa umetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la mifumo kusomana na kubadilishana taarifa.

Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla leo Agosti 27, 2024 baada ya kuzindua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali kinachofanyika katika Hoteli ya Kibo Palace jijini Arusha.

Amesema Wizara hiyo imeelekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mfumo huo kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambao utawezesha mifumo ya TEHAMA ya kisekta kusomana na kubadilishana taarifa utakaojumuisha moduli tatu ambazo ni Jamii Namba, Jamii Kadi na Jamii Malipo.

“Tunategemea mradi huu ukikamilika kila mtanzania atakuwa na Jamii Namba ambayo ni namba ya NIDA itakayokuwa ndio utambuzi wa kila mtanzania na kumwezesha kupata huduma za kijamii”, amesema Bw. Abdulla na kuongeza;

"Baada ya kila mtanzania kupata Jamii Namba, Serikali itaitambulisha Jamii Kadi ambayo itakuwa ni kadi ya kielektroniki itakayojumuisha huduma kadhaa za kielektroniki ndani ya kadi moja kwa sababu itaunganisha taarifa za kadi za benki, vitambulisho vya kitaifa, kadi za kusafiria, bima na nyingine nyingi".

Amefafanua kuhusu Jamii Malipo kuwa ni programu itakayotengenezwa na kuunganishwa na Jamii Kadi na pia itaunganishwa na Mfumo wa Malipo ya Haraka Tanzania (TIPS) unaoruhusu miamala kufanyika kielektroniki kati ya benki na taasisi mbalimbali za kifedha nchini Tanzania.

Ameongeza kuwa kupitia Jamii Malipo kila mwananchi ataweza kufanya miamala kupitia akaunti yake ya benki, M-Pesa, Airtel Money, Paypal na nyingine nyingi kwa kutumia Jamii Kadi, simu ya mkononi au kompyuta ikiwa ni pamoja na kufanya manunuzi na kulipia huduma mbalimbali za kijamii.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: