Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba akitoa wasilisho la hali ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara ya Mawasiliano kwa Mkoa wa Mwanza mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Nape Moses Nnauye (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza, Wakuu wa Taasisi na watoa huduma tarehe 18 Julai, 2024 kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Sengerema, Wilaya ya Sengerema.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Mwanza.
Jumla ya Shilingi Bilioni 2.44 ikiwa ni ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), zimetumika kujenga minara 17 katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mwanza.
Hayo yamebainishwa tarehe 18 Julai, 2024 na Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi Justina Mashiba, wakati akitoa taarifa ya utendaji wa Mfuko huo na hali ya Mawasiliano katika Mkoa wa Mwanza kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb.), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda na viongozi wengine.
Bi. Mashiba amemwambia Waziri Nape na viongozi hao wa Mkoa kwamba, minara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 inayojengwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, itakayowanufaisha watu Milioni 8.5 nchi nzima.
Amesema, minara hiyo 17 mkoani Mwanza, itawawaunganisha na Tanzania ya kidigitali Wananchi 296,410 waliopo katika vijiji 52 vya kata 16 na hadi mwishoni mwa Juni 2024, minara 7 imekwishawashwa.
Akizungumzia Wilaya ya Sengerema Bi Mashiba amesema minara miwili katika vijiji vya Sotta Kata ya Igalula, na kisiwa Lyakanyasi Kata ya Chifunfu itakayonufaisha wananchi zaidi ya elfu 30.
Bi. Mashiba amesema, vijiji vilivyonufaika na minara hiyo 17 ni iliyojengwa na watoa huduma kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G, vijiji hivyo vipo katika kata za Nyamhongolo, Sangabuye, Shibula, Kandawe, Lubili, Chifunfu na Igalula.
Akielezea hali ya mawasiliano mkoani Mwanza, Mashiba amesema, minara 50 ilikwishajengwa mkoani humo kupitia ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia UCSAF ya Shilingi Bilioni 6.69 na kuwanufaisha Watanzania wa Vijijini 885,420.
Picha mbalimbali za matukio wakati Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Nape Moses Nnauye (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza, Wakuu wa Taasisi na watoa huduma tarehe 18 Julai, 2024 wakati wakipokea taarifa ya hali ya Mawasiliano katika Mkoa wa Mwanza kutoka Viongozi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Sengerema, Wilaya ya Sengerema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakili John Daffa akitoa wasilisho la hali ya huduma ya mawasiliano kwa Mkoa wa Mwanza amesema kwa ujumla Minara 422 inatoa huduma za mawasiliano kwa teknolojia zote 2G, 3G na 4G.
Wakili Daffa amesema watumiaji wa mawasiliano wameongezeka kwa zaidi ya asilimia 42.25 kutoka Juni 2022 hadi Machi 2024 na kwamba usajili wa line za simu kimkoa Mwanza umeongezeka kwa asilimia 6.
Toa Maoni Yako:
0 comments: