MKUU wa mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga leo mapema akiwa kwenye ziara yake katika Mji mdogo wa Mererani Wilayani Simanjiro, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Naepo iliyopo katika Kata ya Naisinyai kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili 2024 mradi uwe umekamilika na unaanza kufanya kazi.
Zahanati ya Naepo inajengwa kwa fedha kutoka vyanzo mbalimbali ambapo shilingi Mil. 50 ni fedha za mapato ya ndani, Mil. 48 fedha za nguvu za Wananchi na Mil. 20 ni fedha ambazo zimechangiwa na mdau hivyo kufanya jumla ya Shilingi Mil. 118.
Vilevile Mhe. Mkuu wa Mkoa ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Sokoni Mirerani - Mgodini Tanzanite kilomita 1.2 kwa kiwango cha lami inayotekelezwa na Mkandarasi M/S EMMA & SONS CONTRACTORS LTD. Mradi huu ulitengewa jumla ya shilingi milioni 898 hadi kukamilika.
Katika hatua nyingine, Mhe. RC Sendiga amemuagiza na kumpa mwezi mmoja Meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro kusimamia na kuhakisha mradi huo uwe umeshakamilika alipotembelea mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za tozo ya mafuta.
Miradi mingine ambayo imetembelewa na Mhe. Mkuu wa Mkoa ni pamoja na ujenzi wa Soko la madini, mradi unaotekelezwa kwa fedha shilingi Bilioni 5.43 na hadi sasa mradi upo katika asilimia 80 (80%) ya utekelezaji. Mradi mwingine ni ujenzi wa kituo cha Afya cha Tanzanite kilichopo kata ya Mirerani. Mradi huu umetengewa fedha kutoka Serikali kuu shilingi milioni 500 kujenga jengo la wagonywa wa nje (OPD), Maabara na jengo la mama na mtoto. Mradi huu upo katika hatua ya msingi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: