Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva akiwemo Harmonize, Marioo, Sholo Mwamba, Balaa Mcee, Sarafina, Mimi Mars, Mzee wa Bwax wameungana na umma wa Mtwara kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya chanjo ya UVIKO-19 katika uwanja wa Nyangwanda Sijaona.. Tukio hili limeandaliwa na Wizara ya Afya kupitia kitengo cha Elimu kwa Umma, pamoja na FHI 360 kupitia mradi wa EpiC kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Malengo ya nchi ni kuchanja asilimia 70% ya wananchi wake kufikia mwishoni mwaka 2022, Mpaka kufikia tarehe 10 Julai Mtwara ilikuwa imechanja asilimia 29.3% ya wananchi wake . “Tunashukuru sana Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani kwa uamuzi wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 na magonjwa mengine” alisema Ummy Mwalimu Waziri wa Afya.
, Wizara ya Afya kupitia kitengo cha elimu ya Afya kwa umma kwa kushirikiana na wadau fhi360 unatumia tukio la kimuziki la Mziki Mnene likiambatana na kauli mbiu ya “Bega kwa Bega, Ujanja Kujanja” kuongeza kasi ya kutoa chanjo ya UVIKO-19.

“Kupitia Kampeni hii tunaendelea kukumbushana kukamilisha dozi, kusajliwa na kupata cheti cha chanjo ili kwa pamoja tufikie malengo ya kuikinga nchi yetu dhidi ya janga hili. Hivyo, ninawashukuru viongozi na wananchi wote mliofika hapa hii leo kushiriki uzinduzi huu pamoja na kuendelea kushirikiana kwa kuhamasishana sisi kwa sisi kutumia chanjo hizi. Vilevile, ninawashukuru FHI 360 na USAID Tanzania kwa kuandaa na kuwezesha shughuli hii.” Alisema Mheshimiwa Ummy Mwalimu.

Katika kuonyesha jinsi wadau wa maendeleo wanavyoshirikiana na serikali kuhakikisha inafikia malengo ya uchanjaji waliojiwekea na mikoa ambamo kampeni ya Mziki Mnene itatekelezwa, mwakilishi mkazi wa FHI 360 nchini Tanzania, Waziri Nyoni alisema; “chanjo ya UVIKO-19 imekuwa ni moja ya mkakati unaotekelezwa kwa msisitizo mkubwa zaidi baada ya kuzinduliwa rasmi nchini na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Julai, 2021. Kutokana na juhudi hizi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, kasi ya maambukizi ya UVIKO-19 imeendelea kupungua nchini. Kampeni ya kuhamasisha chanjo inatarajiwa kufanyika katika mikoa mitano ambayo ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe na Iringa.”

EpiC ni mradi wa kimataifa wa miaka mitano unaotekelezwa na shirika la FHI360 kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) pamoja na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), uliojikita katika kufikia na kuendeleza udhibiti wa janga la VVU/UKIMWI katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni kupitia kutoa msaada wa kitaalamu na huduma za moja kwa moja katika kuondoa vikwazo vilivyopo kufikia 95-95-95, na kuhamasisha usimamizi wa kujitegemea wa miradi ya VVU/UKIMWI kitaifa kwa kuboresha programu za utambuzi wa hali ya maambukizi ya VVU, kinga, matunzo na tiba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: