Na Janeth Raphael
Serikali kupitia jeshi la Zimamoto na Uokoaji imefuta gharama za tozo za ukaguzi wa usalama dhidi ya majanga ya moto katika mashamba ya kahawa, mkonge pamoja na chai.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Agosti 11, Msemaji wa Jeshi hilo, Puyo Nzalayaimisi amesema kuwa pamoja na kufutwa kwa tozo katika mashamba hayo, jeshi hilo pia limefuta tozo hizo katika transfoma pamoja na kushusha tozo iliyokuwa ikilipwa na wachimbaji wadogo kutoka milioni6 hadi laki moja kwa sq mita 0 hadi 200.
Msemaji huyo amesema kuwa mabadiliko ya tozo hizo zilizoanza mwezi Julai, mwaka huu pamoja na kushuka, kumekuwa na maingizo mapya ya tozo ikiwa ni sehemu za karakana, vituo vya usafirishaji na wanaofanya biashara ya kufua nguo ‘dry cleaner’.
“Awali upande wa maduka ulikuwa elfu40 ila kwa sasa tumenyumbua na kuna maduka ya rejareja na jumla. Duka la rejareja ni elfu 20 na duka la jumla ni elfu30. Upande wa saluni ilikuwa ni shilingi elfu40 lakini kwa sasa hivi ni shilingi elfu20,” ameainisha.
Ameongeza kuwa awali jeshi hilo lilibeba jukumu la kumfuata mteja na kuomba kufanya ukaguzi katika jengo, eneo au chombo cha usafiri ila kwa mujibu wa mabadiliko mbalimbali ya kisheria yaliyofanyika, sasa mteja atakuwa na wajibu wa kufika katika vituo na ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika mikoa yao ili waweze kuweka mpango kazi wa kukaguliwa.
Ameongeza kuwa utaratibu huo mpya wa tozo utahusu maduka, viwanda, makazi, ofisi, shule, nyumba za kusihi, usomaji wa ramani pamoja na gharama za usajili wa makampuni yanayojishughulisha na utoaji huduma za kuuza vifaa, uwekaji wa vifaa vya kuzima moto pamoja na mifumo uzimaji moto.
Toa Maoni Yako:
0 comments: