Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana , Ajira na Watu Wenye Ulemavu Pabrobas Paschal Katambi akizungumza na waandishi wa habari wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Keds kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Afisa Rasilimali watu wa Kiwanda cha Keds, Gerald Lyimo akielezea jambo wakati Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana , Ajira na Watu Wenye Ulemavu Pabrobas Paschal Katambi alipotembelea kiwanda hicho.
Na Khadija Kalili Kibaha
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana , Ajira na Watu Wenye Ulemavu Pabrobas Paschal Katambi amesema kuwa ameridhishwa na hali ya uwekezaji aliyoiona kwenye Kiwanda Cha Keds Tanzania Limited kilichopo katika eneo la Lulanzi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Naibu Waziri huyo ametoa pongezi hizo mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kushtukiza kiwandani hapo ambapo wanazalisha taulo za watoto, taulo za kike, sabuni pamoja na vifungashio.
Aidha alitoa Rai kwa Uongozi wa Kiwanda hicho Cha Keds kurekebisha changamoto za utoaji wa hewa chafu ndani ya kiwanda hicho na kurekebisha sehemu mbalimbali ambazo baadhi ya miundombinu yake siyo rafiki kiafya kwa wafanyakazi wake.
Naibu Waziri Katambi alifanya ziara hiyo leo Agosti 10.
Aidha Naibu Waziri Katambi ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge na Mkuu wa Wilaya Sara Msafiri pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja wawekezaji wa Kiwanda hicho ambacho alichokitembelea huku akisema kuwa ameshuhudia uwekezaji wa kiwango cha juu huku kikiwa kimetoka ajira 400kwa Watanzania.
Alisema kuwa wawekezaji ni wajibu wao kufuata sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatoa ajira na kuwalipa kwa wakati wafanyakazi wake kama jinsi wanavyolipwa wafanyakazi wa serikali.
Naye Meneja Rasilimali watu wa Kiwanda hicho Gerald Nicas Lyimo amesema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa nishati ya umeme wa kuaminika pamoja na barabara ya vumbi huku akimuomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwajengea barabara kwa kiwango cha lami ambayo inatumika kuingia na kutoka Kiwandani hapo kwani hivi sasa wanatumia barabara ya vumbi.
"Mkoa wa Pwani ni wa Viwanda hivyo tunaomba tupate umeme wa uhakika na tunaomba tujengewe barabara ya kiwango cha lami sababu inahudumia magari mengi ambayo huchukua malighafi." amesema Lyimo.
Lyimo ameongeza kwa kusema kuwa changamoto nyingine wanayokutana nayo kiwandani hapo ni kutoka kwa baadhi ya vijana wa Pwani kuwa na kasumba mbaya ambapo mara baada ya kupokea mishahara yao huwa hawaonekani kwenye maoneo yao ya kazi hadi baada ya siku nne au tano ndipo hurejea na visingizio lukuki jambo ambalo linakatisha tamaa wawekezaji hivyo
amemuomba Naibu Waziri huyo kuandaa makongamano yatakayowakutanisha vijana wa Pwani na kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kuthamini ajira.
Toa Maoni Yako:
0 comments: