Na. Damian Kunambi, Njombe
Kutokana na kuwepo kwa changamoto ya umeme unaozalishwa na kampuni ya madope Hydro inayomilikiwa na kanisa jimbo katoliki Njombe serikali kupitia waziri wa nishati January Makamba imesema ipo tayari kuununua umeme wote (MW 1.7) unaozalishwa katika mradi huo wa umeme endapo wamiliki wa mradi wataridhia kufanya hivyo.
Waziri Makamba ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliohusisha viongozi mbalimbali wa chama na serikali na kuongeza kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakaponunua umeme huo kutawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika kwani kwa sasa katika megawati 1.7 zinazozalishwa, umeme unaotumika ni 0.3 tu.
Amesema wataalam wa TANESCO watafika Lugarawa tarehe 7 Agosti 2022 ili kufanya tathmini ya Miundombinu ya Usafirishaji umeme pamoja na kusaini mikataba ya makubaliano na wamiliki wa mradi huo hivyo ni mategemeo kuwa ifikapo mwezi February mwaka 2023 wananchi hao watakuwa wameshaanza kupata umeme wa uhakika.
Aidha kwa upande wake mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema kuwa, wananchi wamekuwa wakipata tabu na hasa wanawake ambapo wanahangaika kusaga unga na mafuta ya alizeti kutokana na mgao huo.
Ameongeza kuwa kuna baadhi ya vijiji havijafikiwa kabisa na umeme huo, kama kijiji cha Lusala na Utilili vya kata ya Lupanga, baadhi ya vitongoji vya kata ya Mlangali ambapo wananchi waneshasuka nyaya lakini bado hawajafikiwa na umeme pamoja na kata ya madope ambapo kuna vijiji vitatu navyo havijafikiwa na umeme.
Aidha kwa upande wake mkurugenzi ofisi ya maendeleo jimbo katoliki Njombe Padri Hermegrid Lugome amekiri kuwepo kwa changamoto katika mradi huo na amesema wao wapo tayari kuachia mradi huo kwenda serikalini hivyo wataalam watakapofika watawaonyesha ushirikiano wa kutosha.
" Kwakweli huu mradi unatusumbua sana na kutuchosha, natamani hata kesho hao wataalam waje maana naona hiyo tarehe 7 ni mbali", amesema Lugome.
Toa Maoni Yako:
0 comments: