Anaandika Dkt. Hassan Abbasi, KM-USM.

Ikisiri: andiko hili linafanya tamathali na balagaha ya visa viwili vilivyotokea Southampton, April 14, 1912 na Birmingham, Julai 30, 2022:

Naam sasa tuanze simulizi hii…

Katika hotuba yake siku anawapokea mabinti wa Serengeti Girls Ikulu, Dar es Salaam, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kujituma walikoonesha mabinti wale, wakipambana na kupangua hila mbalimbali, Rais alisema Tanzania ni Jamhuri ya watu wenye kupambana.

Miaka kadhaa nyuma kabla ya kauli hii, taswira inanijia, jinsi wapambanaji hodari wa nchi hii kuanzia waliopinga ukoloni kwa fimbo, mishale, mikuki yao na hata kwa kutumia viumbe hai wanaotuzunguka (mfano teknolojia ya nyuki aliyoitumia Malkia Liti wa Singida) hadi viongozi waliotumia diplomasia ya lugha na hoja kama Mwalimu Nyerere wa Butiama.

Katika lindi hili la mawazo na tukiwa tunafurahia medali ya fedha ya shujaa mwingine Alphonce Simbu kule Birmingham, anaibuka binti huyu Jackline Sakilu anayetekeleza kivitendo kauli ya Rais kuwa nchi hii ni Jamhuri ya Wapambanaji. Na hakika ni hivyo iwe kihistoria, kijiografia na hata kijionolojia!

Naungana na Rais na nilifurahi sana aliposema vile siku ile kwa sababu hili ni la hakika kwani kiasili na kihistoria Tanzania si Taifa la ndonga laini za Mandonga, au akili legelege wala nyoronyoro za wanaowaza mbele tu na si mbali, wala lenye haiba ya mambo ya kusadikika bali lenye watu kuanzia wanyonge, mabarobaro, maajuza na mashaibu waliothabiti (ingawa pia wanafiki na wasaliti wachache kama akina Mangungo hawakosekani. Twende nao tu. Hakuna namna. Wapo tu).

Ninapokumbuka hivi kuhusu mchango wa mashujaa kutoka miongoni mwa maajuza na mashaibu wetu katika kila nyanja, kinakuja kisa cha mwanariadha Shaibu John Stephen Akhwari ambaye katika mashindano ya Olimpiki kule Mexico City mwaka 1968 aligoma kujitoa baada ya kuumia akikimbia na akajiburuza hadi kumaliza mbio saa kadhaa baadaye watu wengi wakiwa wameshaondoka. Naiona chemchem ya ushujaa ikiendelea!!

Jackline naye, jana Julai 30, 2022, ikiwa ni takribani siku 25 tangu Rais Samia akumbushie ushujaa na upambanaji wa Watanzania, na ikiwa ni takribani miaka 54 tangu Shaibu Akhwari naye aweke rekodi Mexico, sasa naye ameendeleza ushujaa ule.

Katika asubuhi iliyoamka ikiwa tulivu kule Birmingham lakini kiupepo kikipepea kwa mwendo wa taratibu kule Kizimkazi na majahazi yakirejea ufukweni kule Msimbati, Jackline anayaanza mashindano ya marathoni kilometa 42 jijini Birminghm, Uingereza na kwa kilometa kadhaa akionekana akiwa katika ari ya ushindi na hata mara kadhaa wakionekana yeye na mkimbiaji mwenzake Failuna Matanga wa Tanzania wakipeana ishara za jinsi ya kuzidi kwenda mbele!

Ghafla km 14 hivi baadaye, kama ambavyo meli iliyosheheni fahari ya Titanic ilivyokutana na mwamba wa barafu (iceberg) usiku wa April 14 na kisha asubuhi ile ya April 15, 2012, Jackline naye anapata dhoruba ya aina yake.

Ingawa Titanic yenyewe ilitokea Southampton, Jackline yeye tatizo lake limetokea Birmingham, na kama Titanic ilivyoanza kwa matumaini tele, Jackline naye alianza kwa matumaini tele na akawa anapambana kwenda mbele kisha ghafla hali inakuwa ya fashtiti lakini anagoma kupatwa na jakamoyo lililoikumba Titanic.

Kama ilivyokuwa saa chache tangu ianze safari kwa Titanic, Jackline naye kilometa 17 hivi kati ya 42 kwa uchungu, huzuni na ikionekana dhahiri imemsumbua kiasi, anarejea nyuma katika mapambano ya medali!

Anarejea nyuma kidogo na mwenzake Failuna anajaribu kumshawishi waende lakini inashindikana kwani maumivu ni makali, Failuna analazimika kuongeza mwendo na kuondoka na wakimbiaji wengine, Jackline anabaki nyuma akiugulia maumivu lakini anafanya jambo kubwa na la kihistoria.

Titanic ilizama takribani saa mbili na ushee baadaye tangu ianze safari na tangu ipate dharura, Kuna kitu Jackline anakifanya saa mbili baadaye na ushee!

Hiki si kisa cha Titanic lakini naomba nivute hapa pia kidogo katika kisa cha filamu ya “No Retreat, No Surrender,”.

Sikiliza, Jackline Sakilu, anakubali “kuretreat” (kurudi nyuma) lakini hakubali “kusurrender” (kusalimu amri).

Kwa pale Birminghan angeweza tu kujitoa na Jackline angepokewa na wahudumu na wasaidizi ambao wangempa sharubati na chokoleti kisha akapelekwa kwenye kliniki nzuri za samawati!

Lakini hapana! Sikia hii tena kwa Sikilu ni hapana; akakumbuka jinsi Rais wake alivyosisitiza kuhusu Jamhuri ya Wapambanaji.

Akakumbuka jinsi Rais wake huyo huyo ndani ya mwaka mmoja akiwa madarakani na akiwa bado anajipanga lakini akatoa fedha za kuwezesha, kwa mara ya kwanza, kambi ya kujiandaa na Commonwealth kuanza tangu Februari wakati mashindano ni Julai mwishoni!

Naamini na nausoma hivyo moyo wake, akakataa yote hayo akasonga mbele!

Jackline, kama Shaibu Akhwari alivyosema mwaka 1968 “sikutumwa mile 5,000 na nchi yangu kuja kushiriki bali kumaliza mbio,” naye akasonga mbele, akapata maumivu makali, akayavumilia kwa ajili ya Tanzania na hatimaye ikawa kilometa 20, ikawa kilometa 30, ikawa kilometa 40 na mwisho 42 akafanya jambo.

Nimesema hapo juu, Titanic ilizama siku ile ya asubuhi ya April 15 ikiwa ni saa mbili hivi na ushee tangu ipate dhoruba usiku wa April 14, Jackline alikataa kuzama na kwake saa mbili na ushee badaye tangu washindi wapatikane, akafika eneo la mwisho la kumalizia mbio, wazungu wakimshangilia, kamera zikimmulika na ndipo hapo akawa tayari kupokewa na wahudumu madhubuti, kukubali kiti chao, sharubati zao na kupelekwa kwenye kliniki zao za samawati!!

Wenzetu wazungu wamempokea kama shujaa na hawakumchukulia poa, naiona Tanzania inaanza kugawanyika, wapi wanaomchukulia Jackline poa lakini mimi nawaambia tunakosea.

Kwangu mimi hili litabaki kuwa tukio mojawapo kubwa la kishujaa kwa mwaka huu nchini.

Ni kosa kuliona jambo hili kama la kawaida au la kuiga. Hapana. Hapana. Hapana.

Si la kawaida; tuache hizi mambo, tunashida ya kuiona kila kawaida ni kawaida lakini hii amini nawaambia hata kama bado utataka kuiona ni kawaida nakwambia hii hapana, sio kawaida ya kawaida!

Huyu ni shujaa wetu na wa zama zetu, na kwa maoni yangu, ni mshindi wetu mwingine wa medali hata kama sio dhahabu au fedha.

Ungana nasi siku wanayorudi tumpe medali shujaa huyu. Kwangu mimi tuna medali mbili za marathon Birmingham mpaka sasa; ya Sajini Alphonce Simbu na ya sada yetu Jackline Sakilu

Wakatabahu.

Wassalam

Kutoka Kichangani, Hale Mwakinyumbi.

Julai 31, 2022.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: