Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewashauri viongozi wa Dini nchini kufuata sheria na kanuni zilizopo katika kusimamia majukumu yao.

Mhe. Hemed alieleza hayo Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar alipokutana na kufanya mazungumzo na kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini iliyo chini ya Mwenyekiti wake Mufti Mkuu wa Zanzibar.

Alisema kuna haja kwa viongozi wa Kamati hiyo kusimamia sheria hasa kwa kuzingatia Imani za Dini ili kuwa karibu Mweenyezi Mungu jambo ambalo litapelekea kuwa na jamii iliyonyooka.

Alisema sio jambo la kuridhisha kwa baadhi ya watu wenye nia mbaya kwa kujivika vazi la viongozi wa Dini hali ya kuwa kamati inayotambulika kisheria ipo chini ya usimamaizi wa ya Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar alieleza kwamba serikali inathamini mchango unaotolewa na kamati hiyo na itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano ili kuhakikisha inaendelea kufanya kazi vyema.

Mhe. Hemed aliwakumbusha viongozi hao kutumia nafasi waliyonayo katika jamii kwa kuendelea kutumia viriri kwa kuhubiri Amani hasa katika maeneo yao ya Ibada akieleza kuwa jamii inawaamini na kuwasikiliza viongozi hao.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed alisema maendeleo katika nchi yoyote lazima pawe na Amani na kueleza kuwa Serikali imekuwa ikihamasisha suala la Amani na utulivu ambapo hadi sasa wananchi wamekuwa waelewa katika kulinda tunu hiyo na kwa sasa serikali inaendeleza kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mchungaji Shukuru Maloda alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa kamati hiyo inaunga mkono serikali katika kupiga vita masuala ya udhalilishaji ambapo mwaka 2022 wameandaa mkakati madhubuti utakaoanza kwa wilaya ya Kati na wilaya ya micheweni wa kuhakikisha vitendo hivyo vinapungua katika maeneo hayo.

Nae Mjumbe wa kamati hiyo shekh Thabit Nouman Jongo alieleza kuwa miongoni mwa kazi za kamati hiyo ni pamoja na kutatua migogoro katika Jamii pamoja na kuhamasisha Amani.

Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Zanzibar imeanzishwa rasmi mwaka 2005 chini ya Aliekuwa Mufti Mkuu wa Zanzibar Marehemu Shekh Harith Bin Khelef.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: