Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula akiongea na wadaiwa sugu na kutoa ufafanuzi wa msamaha wa kodi kwa taasisi za dini.
Baadhi ya wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi wakimsikiliza Mh.Dkt. Angeline Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi alipofika mkoani Singida kuzungumza nao.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula akipata maelezo kuhusu nyumba zinazopangishwa na Shirika la Nyumba la Taifa NHC
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula akiza katika picha ya pamoja na watumishi wa ofisi ya Ardhi ya Mkoa ya Singida mara baada ya kumaliza Ziara yake mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Angeline Mabula amefanya ziara ya siku moja Mkoani Singida kwa lengo la kukukutana na wadaiwa wenye madeni ya muda mrefu (wadaiwa sugu), kujadili changamoto zao na kutafuta suluhisho kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.

Naibu Waziri Mabula amechukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara zake katika mikoa mbalimbali nchini kufuatilia makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na kutatua changamoto zake. Awali wakati akipata taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mkoa, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Shamim Hoza pamoja na timu yake walimueleza Naibu Waziri kuwa kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wadaiwa “kukingiwa kifua” na viongozi.

“Lengo la kuja hapa kuongea na ninyi leo ni kujua hii sintofahamu juu ya ulipaji kodi, kumekuwa na changamoto za ulipaji ambapo watumishi wetu wamekuwa wakikwamishwa na baadhi ya wamiliki kukimbilia kwa viongozi ili wawatetee wasilipe kodi, naomba niwakumbushe kwamba, wanachelewesha tu lakini kodi ya serikali ni lazima ilipwe. Ningeomba kwa upande wa viongozi kuanzia Wizara, Mkoa na Wilaya tufanye kazi kama timu katika kuhakikisha kodi inakusanywa badala ya kukwamisha” Alisema Naibu Waziri.

Moja kati ya makundi ambayo yalijitetea kushindwa kulipa kodi kwa wakati ni pamoja na taasisi za dini zilizojitetea kuwa hazijiendeshi kwa faida na kwamba zingeomba kupata msamaha wa kodi. Pia kundi hilo lilihitaji ufafanuzi kutoka kwa Naibu Waziri kwa maelezo kwamba serikali ilitoa msamaha wa kodi mwaka 2018 kwa asasi za huduma zisizojiendesha kwa kutengeneza faida.

Akilielezea kwa kina suala hilo, Naibu Waziri Mabuka alisema, msamaha uliotolewa ni ule unaohusu ile huduma ya dini yenyewe, kwa maana ya kanisa au msikiti, lakini kama vyombo hivyo vimeanzisha huduma nyingine ambazo wanawalipisha wananchi basi ni lazima majengo ya huduma hizo yalipiwe kodi.

“Niweke wazi kwamba kama wewe unaendesha kanisa, serikali imetoa msamaha kwa jengo hilo tu, ila pale utakapoendeleza kutoa huduma zingine ambazo mtawalipisha wananchi kama vile shule, hospitali na vitu kama hivyo basi ni lazima huduma hizo zilipiwe kodi. Ila kama unatoa huduma hizo bure kabisa uje kwa Kamishna utajaza fomu maalumu na akijiridhisha utaombewa msamaha kwa huduma hiyo” Aliongeza Naibu Waziri.

Wakati huo huo, Naibu Waziri ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha linawapitia wapangaji wote Mkoani Singida na kujiridhisha kuwa ni wapangaji halali. Hii inatokana na kujitokeza kwa hali ya wapangaji walio na mikataba na NHC kupangisha watu wengine. Zoezi hili tayari limeshafanyika Dar es salaam ambapo wapangaji waliokutwa wamepanga kupitia wapangaji wenye mikataba na Shirika la Nyumba la Taifa waliondolewa au kupewa mkataba kama wapangaji halali wa nyumba hizo.

Singida ni moja ya Mikoa yenye madeni sugu yanayohusisha wafanyabiashara, asasi zisizo za kiserikali pamoja na Taasisi za Serikali ambapo hadi kufikia tarehe 15 Aprili mwaka huu Ofisi ya Kamishna Msaidizi Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Halmashauri za manispaa ilisambaza hati za madai 679 zenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.3 ambapo kati ya hati hizo wadaiwa 213 wanaodaiwa wameshafikishwa katika mahakama za Mabaraza ya Ardhi.

 Imeandaliwa na Lusajo Mwakabuku, 
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, 
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: