MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi wa Ukanda wa Pwani mikoa ya Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, kisiwa cha Mafia pamoja na kisiwa cha Unguja na mkoa wote wa pwani kuchukua tahadhari ya upepo mkali ambao unatarajiwa jumapili ya Aprili 25 ambapo kimbunga Jobo kinatarajiwa kutua Dar es Salam.

Imeelezwa, kufikia Aprili 25, 2021 Kimbunga 'Jobo' kinatarajiwa kutua jijini Dar es Salaam kikiwa na upepo mkali wa kufikia kilometa 60 kwa saa ambao unaweza kuleta athari kwa jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, DK Agness Kijazi amesema hayo Ijumaa Aprili 23, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uwepo wa kimbunga Jobo kilichopo umbali wa kilometa 235 kutoka mashariki mwa kisiwa cha Mafia kilichopo mkoani Pwani.

Amesema kufikia Aprili 25 mwaka huu kimbunga hicho kitakuwa tayari kimetua jijini Dar es Salaam kadri mwelekeo unavyoonyesha lakini kinatarajiwa kuendelea kupungua nguvu na kuwa na mgandamizo mdogo wa hewa kikiwa katika Mwambao wa Pwani ya Tanzania.

" Vipindi vya upepo mkali unaofikia kilometa 50 hadi 60 kwa saa, mawimbi makubwa baharini pamoja na ongezeko la mvua kwa maeneo ya Ukanda wa Pwani vinatarajiwa kujitokeza huku maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja ni Mikoa ya Pwani, ikiwemo nm kisiwa cha Mafia, Lindi, Dar ea salaam na Kisiwa cha Unguja Mtwara, Tanga na kisiwa cha Pemba.

Kimbunga Jobo kina nguvu, licha ya kupungua nguvu kadri kinavyosogea lakini bado nguvu hiyo ni kubwa na inaweza kuleta arhari kwa sababu sasa hivi nguvu yake kwenye upepo ni kilometa 90 kwa saa na tunatarajia mpaka kikitua Dar es Salaam kitakuwa na kilometa 60 kwa saa upepo ambao ni mkubwa na unaweza kuleta athari," amesema Dk. Kijazi.

Dk Kijazi amesema njia yote ya kimbunga chenyewe kinaonekana kitakuwa kwenye eneo kubwa hivyo eneo la ukanda wa Pwani linatakiwa liwe la tahadhari kwa kuwa kimbunga kilianza kwa mwendo kasi kilometa 20 kwa saa.

DK Kijazi amesema wameona kwenye Setilaiti maeneo ya Magharibi katika ziwa Victoria kuna mawingu mengi kutokana na kuna unyevunyevu kutoka msitu wa Kongo na kuvutwa maeneo ya nchi nzima.

DK Kijazi amesema uwepo wa kimbunga Jobo unatarajiwa kuendelea kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa na kusababisha ongezeko la vipindi vya mvua kwa maeneo yaliyombali na ukanda wa Pwani ikiwemo Ziwa Victoria.

Hata hivyo, wananchi wameshauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutola Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kupata ushauri n miongozo ya wataalamu katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: