Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Women Wake-up (WOWAP) Issah Shayo, akimkabidhi vipeperushi hivyo Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Sabasaba, Grace Benjamini kwa niaba ya walimu wa shule hiyo.
Afisa Utawala wa Shirika hilo, Loveness John, akitoa Elimu ya Uraia ya Mpiga Kura kwa Walimu wa Shule ya Msingi Sabasaba.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Women Wake-up (WOWAP) Issah Shayo, akimkabidhi vipeperushi hivyo Msaidizi wa Meneja wa Kampuni ya Simu ya Airtel, Remmy Aloyce kwa niaba ya wenzake. Kulia ni Afisa Utawala wa WOWAP, Loveness John.
Afisa Utawala wa WOWAP, Loveness John, akitoa Elimu ya Uraia ya Mpiga Kura kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida (Mandewa)
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida.
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP) limekumbusha jamii kuhakikisha ifikapo Oktoba 28 mwaka huu kila mwenye sifa ya kupiga kura ajitokeze na kadi yake ya kupigia kura katika kituo alichojiandikisha ili kutimiza haki yake ya msingi ya kikatiba
Aidha, shirika hilo limesisitiza umuhimu wa kila mtanzania kuzingatia misingi ya amani na utulivu wakati mchakato huo ukiendelea, ikiwemo kufika mapema kituoni kupiga kura na kuondoka kuendelea na majukumu mengine kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, ili kuepusha madhara au viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza
Afisa Utawala wa WOWAP, Loveness John aliyasema hayo kwa nyakati tofauti jana wakati akielimisha na kukumbusha jamii mkoani hapa juu ya namna bora ya kufanikisha Uchaguzi wa mwaka huu
“Mafanikio ya uchaguzi wa mwaka huu yatatokana na ushiriki wenu, niwasihi sana jitokezeni kwa wingi siku ya octoba 28 ili kwa pamoja tutimize haki ya msingi nay a kikatiba ya kuchagua viongozi bora kwa hatma ya maisha yetu na Taifa letu…’Kura yako ni Sauti yako’,” alisema John
Akizungumza na watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Singida, Makampuni ya Mitandao ya simu (Tigo na Airtel) Hospitali ya Mkoa na Rufaa, walimu wa shule ya Sekondari Senge na shule za msingi Sabasaba na Bomani, Afisa Utawala huyo, alisema kila mdau akitimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa basi watanzania wataweza kupiga kura kwa amani siku hiyo ya uchaguzi
Kwa upande wake, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka WOWAP, Issah Shayo, aliwatoa hofu wapiga kura wote wenye mahitaji maalumu, akisisitiza kuwa tayari maelekezo yametolewa kwa watendaji wote wa uchaguzi kutoa kipaumbele vituoni kwa watu wenye ulemavu, wajawazito, wazee, wagonjwa na akinamama wanaonyonyesha
Shayo alisema kwa wale wasiojua kusoma na kuandika ruksa kwenda na watu wanaowaamini kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura, lakini pia kumewekwa utaratibu madhubuti na utakaokuwa na tija kwa watu wa makundi maalumu, katika kuhakikisha wote wenye sifa ya kupiga kura wanafanya hivyo, lengo ni kuufanya uchaguzi wa 2020 kuwa wa kuaminika, kwa uwiano na mazingira sawa.
kwa wiki mbili mfululizo limeendelea kusambaza elimu ya uraia ya Mpiga Kura kwa wananchi wote wa mkoa wa Singida na vitongoji vyake, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwana-singida anatumia haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi sahihi kuelekea uchaguzi mkuu
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka WOWAP, Issah Shayo alisema azma hasa ya mafunzo hayo ni kuelimisha na kuwakumbusha wananchi juu ya wajibu wao muhimu wa kuhakikisha wanachagua viongozi bora kwa maendeleo yao katika muktadha wa kauli mbiu isemayo ‘Kura yako, Sauti yako’
“Tunawasihi wananchi wote wa Singida, ifikapo Oktoba 28 twendeni tukapige kura ili kupata viongozi watakaoamua mustakabali wa maisha yetu na vizazi vyetu…kumbukeni kura yako ndiyo sauti yako,” alisema Shayo
Alisema shabaha ya mafunzo hayo ni kuhamasisha na kuchochea kasi ya ongezeko la wananchi wengi zaidi kutambua haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa kwa uratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Mpaka sasa shirika hilo linaendelea kutoa mafunzo hayo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye majimbo ya Singida Mjini, Singida Vijijini, Singida Kaskazini, Singida Magharibi, Manyoni Mashariki, Iramba Mashariki na Magharibi
“Tunapita kwenye mikusanyiko na kufanya mikutano na wananchi na kuwapatia elimu hii ya uraia, na tunashukuru kila tunapopita mwamko ni mkubwa. Ujumbe wetu mkubwa kama shirika la WOWAP ni kuwasihi wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura wasipoteze fursa hiyo muhimu ifikapo Oktoba 28,” alisema Afisa Utawala wa Shirika hilo, Loveness John.
Toa Maoni Yako:
0 comments: