Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mkono na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa mara baada ya uzinduzi rasmi wa jengo la abiria (Terminal 3) la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Na Mwandishi Wetu.
RAIS Dkt. John Magufuli amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini pasipo na kutegemea fedha zenye masharti zinazotolewa kutoka kwa wafadhili na wadau wa kimataifa wa maendeleo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Jengo la 3 la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi (Agosti 1, 2019), Rais Magufuli alisema uzinduzi wa Jengo la Uwanja huo ni ushahidi wa wazi wa usimamizi na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali zinazotokana na kodi ya wananchi.
Aliongeza Jengo la Uwanja huo limejengwa kwa asilimia 100 kutokana na kodi za Watanzania, na hivyo kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) kusimamia vyema miundombinu ya Uwanja huo kwa kuhakikisha kuwa inatunzwa ili kuakisi vyema taswira ya Jiji la Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema jengo hilo litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia jumla ya abiria Milioni 6 kwa mwaka limeigharimu Serikali kiasi cha Tsh Bilioni 722 ambazo ni fedha zilizotolewa na Serikali, limeweza kuifanya Serikali kuaminika na kuwa na udhubutu wa kutekeleza miradi ya Maendeleo kupitia fedha za ndani.
“Ipo miradi mingi ya Maendeleo tunayoisimamia kwa fedha zetu za ndani ikiwemo Ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa kufua umeme Mto Rufiji, Barabara za Juu Ubungo, Daraja la Kigongo-Busisi, Daraja la Salender, Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege 15, kujenga rada 4 katika Viwanja vya Ndege vya Dar Salaam, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro, huu ni ushahidi wa usimamizi imara wa fedha zetu za ndani” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya anga nchini, kwa kuwa sekta hiyo imekuwa kiungo muhimu katika maendeleo ya sekta ya Utalii, kwani kila siku takribani watu Milioni 12 duniani hutumia usafiri wa anga kutokana na kuwa njia ya haraka na ya uhakika kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutoa kipaumbele kwa makampuni ya kitanzania yanapewa nafasi katika maduka yatakayofunguliwa ndani ya Uwanja huo ili kuwawezesha kufaidi matunda ya kodi yao sambamba na kuweza kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema tangu mwaka 2004-2011 Serikali imechukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya majengo ya Uwanja wa ndege vyaJulius Nyerere ikiwemo ujenzi wa Jengo jipya la tatu la abiria katika uwanja huo, kutokana na majengo ya sasa ya jengo la I na II kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uwezo mdogo wa kuhudumia abiria.
Anaongeza kuwa ujenzi wa Jengo hilo la tatu la abiria lilisimama ujenzi wake mwaka 2016 kutokana na mkandarasi kudai Tsh Bilioni 29, ambapo awali alishapokea kiasi cha Tsh Bilioni 380 kati ya Tsh Bilioni 560 zilizohitajika kwa ajili ya ukamlishaji wa jengo hilo hapo awali, lakini mwaka 2017 Serikali ilitoa zabuni ya ujenzi wa mradi huo kwa mkandarasi mwingine kutokana mkandarasi aliyepita kuwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mfugale alisema kutokana na kasoro zilizojitokeza, shughuli za ujenzi wa jengo hilo zilipelekwa kwa kampuni ya TECU na mshauri mwelekezi kampuni ya Arab Contractor ambapo hadi kufikia Mei 29 mwaka huu zilikamilisha ujenzi wa jengo hilo na kusubiri kukabidhiwa kwa Serikali kwa ajili ya kuanza kutumika kwake.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama alisema hadi kufikia sasa jumla ya makampuni 18 kati ya 23 ya kimataifa tayari yamehamishia shughuli zao katika Uwanja huo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za usafiri kwa abiria wanaosafiri kwenda nje ya nchi.
Aliongeza kuwa katika kuimarisha usimamizi bora wa Jengo la Uwanja huo, Mamlaka hiyo pia imewapatia mafunzo watumishi wake kwa ajili ya kupata uelewa wa pamoja wa namna bora ya kulinda miundombinu ya Uwanja huo na hadi sasa imepokea Tsh Milioni 500 kutoka Serikalini ilizozilipa kwa mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: