Diwani wa Mwanga Kaskazini (ACT-Wazalendo) Manispaa ya Kigoma Ujiji, Clayton Chipando maarufu Baba Levo amehukumiwa kifungo cha miezi mitano jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumshambulia askari wa kikosi cha usalama barabarani.
Akitoa hukumu hiyo leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019 katika mahakama ya Mwanzo Mwandiga, Hakimu Mkazi, Florence Ikolongo amesema Baba Levo alimshambulia askari F.8350 PC Msafiri Mponela.
Hakimu Ikolongo amesema kifungo hicho ni bila faini.
Karani wa mahakama hiyo, Jackson Mrefu amesema Baba Levo ametiwa hatiani kwa kifungu namba 240 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 chapisho la mwaka 2002.
Kufuatia hukumu hiyo ya kesi namba 52/2019 iliyomtia hatiani Baba Levo ambaye ni msanii wa muziki wa kizazi kipya, katibu wa ACT mkoani Kigoma, Juma Ramadhani amesema chama hicho kinafuatilia na kitatoa tamko.
"Kama chama tumepokea taarifa ya diwani wetu kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano na tumeambiwa kwamba alichukuliwa na gari kupelekwa gerezani, tutatoa taarifa rasmi ya chama leo mchana na jamii itajua msimamo wetu,” amesema Ramadhani
Toa Maoni Yako:
0 comments: