Jeshi la uhamiaji nchini likiwa katika maandamano katika kuadhimisha siku ya kupinga Biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu ambapo amewaonya wote wenye tabia ya kuwarubuni watoto na watu wazima na hatimaye kuwafanya watumwa kuwa sheria inasimamia makali yake, leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kamati ya taifa ya kuzuia na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu Adatus Magere akizungumza katika maadhimisho hayo na kuishauri jamii kutohadaika na mafanikio ya muda mfupi, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola akisalimiana na wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya siku ya kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu ambapo mabalozi na wawakilishi wamevutiwa na kasi ya Tanzania katika kupambana na kukomesha biashara hiyo haramu ya kusafirisha binadamu, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola akipata maelekezo kutoka kwa washiriki wa maonesho walioshiriki maadhimisho ya siku ya kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu duniani ambapo wadau wengi wakiwemo mabalozi wamehaidi kushirikiana na Tanzania katika kupinga janga hilo, leo jijini Dar es Salaam.


WAZIRI wa mambo ya ndani Kangi Lugola ametangaza vita kali dhidi ya watu wanaowarubuni na kuwadanganya watoto na watu wazima kwa kigezo cha kuwapatia maisha mazuri na mwishowe kuwapa malipo duni, mateso na kufanywa watumwa.

Akizungumza leo katika maadhimisho ya siku ya kupinga biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu duniani yenye kauli mbiu ya "Ungana na Serikali Kutokomeza Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, Wahanga Sio Wahalifu Walindwe" yalikofanyika katika viwanja wa Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam Waziri Kangi amesema madhara ya usafirishwaji wa binadamu na kuwatumikisha ni makubwa na hayawezi kufumbiwa macho na hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika zitachukuliwa ikiwepo kutumikia vifungo gerezani.

Amesema ikiwa ni mara ya pili taifa likiadhimisha siku hiyo, malengo kwa mwaka huu ni kuadhimisha siku hiyo kwa kupinga vikali usafirishwaji haramu wa binadamu, kuelimisha jamii kuhusiana na madhara ya usafirishwaji wa binadamu na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika pamoja na kutoa shukrani hasa kwa shirika la uhamiaji la IOM kwa kutoa ushirikiano wa karibu zaidi na Serikali katika kuhakikisha vitendo vya namna hiyo vinakoma.

Waziri Lugola amesema katika kuhakikisha janga hilo linakoma kuanzia Januari 2017 hadi Juni 2019 mafunzo maalumu yametolewa kwa wadau wapatao 600 wakiwemo walezi wa vituo vya waathirika wa usafirishwaji huo, maaskari, mawakili na mahakimu katika kuhakikisha wanapambana na janga hilo katika maeneo yao ya kazi.

Imeelezwa kuwa waathirika wa janga hilo ni vijana, watoto, na wanawake wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24 ambao huchukuliwa kutoka ngazi za Wilaya, Mikoa na taifa na wengine kupelekwa nje ya nchi wakihaidiwa kupewa maisha bora kwa familia zao lakini huishia katika utumwa, kubebeshwa dawa za kulevya, kuuza pombe haramu ya gongo pamoja na kutumikishwa kingono.

Pia ubalozi wa Marekani umetuma ujumbe wa kuipongeza Tanzania kwa kuendelea kupambana na janga hilo la usafirishaji haramu wa binadamu na kuahidi kushiriki katika kutokomeza kabisa janga hilo linaloathiri jamii hasa vijana na watoto katika masuala ya kijamii na uchumi.

Ujumbe huo umeeleza kwamba; "upepo utapita, kwa kuwa usafirishwaji ni wa ndani na nje ya nchi huku asilimia 70 ya waathirika wakiwa ni kutoka ndani ya nchi husika hivyo lazima tupambane kwa kuwalinda vijana na watoto wetu" umeeleza.

Vilevile ubalozi huo umeshauri adhabu kali dhidi ya wahusika na wao kama balozi hapa nchini wapo pamoja katika kupinga janga hilo ambalo sio la asili bali hutengenezwa na kutekelezwa na watu.

Kwa upande wake Mkuu wa shirika la kuwahudumia wahamiaji nchini (IOM) Dkt. Qasim Sufi amesema kuwa usafirishaji haramu wa binadamu umeathiri nchi nyingi hasa katika sekta za kiuchumi huku waathirika wakipata majanga kama magonjwa, vifo na maumivu yanayotokana na harakati za kutengeneza maisha bora kwa familia zao.

Amesema wanawake na watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa janga hilo na amezishauri nchi mbalimbali kuwapokea wahamiaji na kuwapa haki zao za msingi na kibinadamu katika nchi wanazofanya kazi.

Aidha amesema kuwa juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania zinatia moyo na tatizo hilo linaweza kumalizwa kabisa kutokana na uwepo wa wadau wengi wanaopinga usafirishwaji haramu wa binadamu, na kueleza kuwa tafiti zaidi zinaendelea kufanywa zitaisadia Serikali katika kutatua tatizo hilo.

Awali akitoa taarifa ya kamati ya kupambana na usafirishwaji haramu wa binadamu, mwenyekiti wa kamati hiyo Adatus Magere amesema kuwa wahanga wa janga hilo sasa wanajikwamua kupitia fursa zilizopo nchini ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008 mapambano yameshika kasi na waharifu waliokutwa na hatia wengi wao wapo gerezani wakitumikia kifungo.

Ametoa mwito kwa jamii kutohadaika na mafanikio ya muda mfupi na kuwashauri vijana kutumia fursa za nyumbani katika kujipatia maendeleo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: