Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja (kushoto) akibadilishana mkataba wa utekelezaji wa miradi ya majisafi toka kwa wawakilishi wa makampuni ya ukandarasi ya Watanzania na Wachina yatakayotekeleza ujenzi wa miradi itakayojengwa Dar es Salaam na Pwani. Wengine wanaoshuhudia ni Mawaziri, Naibu Waziri, Mwakilishi wa benki ya Dunia na viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/Michuzi TV.
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya utiaji saini wa DAWASA na wakandarasi juu ya ujenzi na uendeshaji wa miradi sita mikubwa ya usambazaji wa maji yenye thamani ya Bilion 114.5 iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Wageni waalikwa na wafanyakazi wa DAWASA wakifuatilia hotuba ya Mhe. Waziri Prof Mbarawa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwasilisha taarifa fupi ya miradi sita mikubwa yenye thamani ya Bilion 114.5 kwa Waziri wa Maji Prof Makame Mbarawa wakati wa halfa iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Miradi hiyo itahudumia maeneo ambayo hayana kabisa mtandao wa DAWASA pamoja na Mkoa wa Pwani.
Wageni waalikwa na wafanyakazi wa DAWASA waliohudhuria hafla hiyo.
Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo akitoa machache.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akifafanua jambo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akielezea furaha yake juu ya DAWASA kupeleka wa maji katika jimbo lake la Mkuranga na vitongoji vyake kupitia miradi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA Jenarali Mstaafu Davis Mwamunyange akielezea chagamoto zinazoikabili mamlaka hiyo.
Wageni waalikwa na wafanyakazi wa DAWASA waliohudhuria hafla hiyo.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Assumpta Mshama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha akitoa salamu.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sophia Mjema ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ilala akitoa salamu.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Kate Kamba akielezea furaha yake jinsi DAWASA inavyotekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kumtua mama ndoo kichwani.
Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo (kushoto) akiteta jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia).
Na Zainab Nyamka na Cathbert Kajuna, Michuzi TV.
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) wametia saini mikataba wa miradi mikubwa sita ya usambazaji maji kwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wenye thamani ya Bilion 114.5.
Utiaji huo wa saini umefanyika leo Julai 2, 2019 katika ofisi za Mamlaka hiyo huku ukishuhudiwa na Waziri wa Maji Prof Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso, Waziri wa TAMISEMI Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Bodi ya DAWASA ikiongozwa na Mwenyekiti Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange na Wakuu wa Wilaya kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Kabla ya utiaji saini, Waziri wa Maji Prof Makame Mbarawa amewataka Mamlaka hiyo kusimamia vizuri miradi yote na kutafuta wakandarasi watakaofanya kazi kwa uweledi na kumaliza kwa wakati na muda mfupi ili wananchi wapate majisafi na salama.
"Mamlaka mnaposimamia vizuri miradi ya maji, na kupata mkandarasi atakayefanya kazi kwa weledi na kumaliza ujenzi wa mradi kwa muda mfupi basi wananchi watapata majisafi na salama," amesema Prof. Mbarawa.
Profesa Mbarawa amesema, li kufikia lengo la serikali la kumtua mama ndoo kichwani kwa asilimia 95 kwa mijini na asilimia 85 kwa vijijini na hilo linawezekana iwapo miradi midogo na mikubwa kusimamiwa vizuri na wakandarasi kumaliza kazi kwa wakati.
Akitoa taarifa fupi ya miradi hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kwa sasa mkoa wa Dar es Salaam unapata maji kwa asilimia 85 na kukamilika kwa miradi hiyo mikubwa itafikia malengo ya serikali ya asilimia 95 kufikia mwaka 2020.
Amesema, katika kutekeleza miradi hiyo fedha zinazotumika ni za ndani zinazotokana na makusanyo ya mapato ya kila mwezi ambapo ndani ya miaka nne wameweza kuongeza ukusanyaji kutoka bilioni 3.2 hadi 11.2 kwa mwezi na asilimia 35 za mapato zinatumika kwenye ujenzi wa miradi ya maji.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA Jenarali Mstaafu Davis Mwamunyange ameeleza changamoto mbalimbali ndani ya mamlaka hiyo ila ameahidi kushirikiana na menejimenti kukabiliana nazo ikiwemo upotevu wa maji na wateja kupewa ankara za maji tofauti na matumizi yao.
Miradi iliyowekewa saini ni mradi wa bomba la kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza wenye wenye urefu wa Km 7.5 na litahudumia maeneo ya Kiwalani Vituka, Buza, Mashine namba 5 - Tandika na Mwanagati na wakazi 173,810 wa kata za Vituka na Buza watapata huduma ya maji kwenye awamu ya kwanza. Mradi mwingine ni mradi wa usambazaji maji utakaoanzia matanki ya Chuo Kikuu mpaka Bagamoyo awamu ya pili, mradi wa kuchimba visima 20 vya Kimbiji Mpera, mradi wa usambazaji maji Kisarawe hadi Pugu, mradi wa maji katika mji wa Mkuranga na mradi wa bomba la kusafirisha maji kutoka Mlandizi (Ruvu juu) hadi Kijiji cha Mboga Chalinze.
Viongozi mbalimbali hususani wawakilishi wa wananchi wameishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwezesha miradi mikubwa kama hiyo kwenda katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Toa Maoni Yako:
0 comments: