Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (katikati) akikata utepe wakati wa uzinduzi wa soko la kimataifa la madini leo jijini Dar es Salaam.
Mfanyabishara ya madini Othman Tharia (kushoto) akitoa maelezo kutoka sekta ya madini mbele ya Mkuu was Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (kulia) mara baada ya kuzindua soko la kimataifa la madini katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (aliyeketi) akisikiliza maelezo kutoka kwa mfanyabishara wa madini Othman Tharia kuhusiana na namna wanavyoendesha biashara hiyo, leo jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda leo Julai 17 amezindua rasmi soko la kimataifa la madini na vito jijini Dar es salaam ikiwa utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kutaka kila Mkoa kuwa na soko hilo.
Akizungumza katika warsha hiyo Makonda amesema kuwa, uwepo wa soko hilo litasaidia Wananchi kununua madini na vito halali na kupunguza matapeli waliokuwa wakiuzia wananchi na raia wa kigeni madini na vito bandia.
Makonda amesema kuwa, uzinduzi wa soko hilo umekuja wakati muafaka ambao Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za SADC ambapo wageni wataanza kuingia nchini mwezi ujao wakiambatana na wafanyabiashara ambapo pia anaamini watapata nafasi ya kutembelea soko hilo na kutengeneza fursa zaidi kwa wafanyabiashara nchini.
Hata hivyo Makonda amesema ndani ya soko hilo yanapatikana madini ya aina zote hivyo amewataka wananchi kulitumia kwakuwa ni halali na linatambulika na serikali.
Kwa upande wake mwakilishi wa wafanyabiashara wa madini nchini Othman Tharia amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa wazo la kujenga masoko hayo ambapo hadi sasa Mikoa 28 imetekeleza kwa kujenga masoko hayo hali itakayopelekea kukoma kwa mianya ya utoroshaji na wakiwa wafanyabiashara wanahaidi kuunga jitihadi za Rais katika utendaji kazi.
Aidha amewataka wafanyabiashara hao kuwa na chama maalumu kitakachowatambulisha kote nchini na wameishukuru Wizara ya madini kwa kusimamia sheria katika usimamizi wa masoko hayo.
Ikumbukwe kuwa Mkoa wa Dar es salaam ndio soko na lango kuu la biashara ikiwemo madini hivyo uwepo wa soko hili ni fursa kwa wachimbaji, wafanyabiashara na wananchi kupata madini na vito halali kwa bei halali.
Toa Maoni Yako:
0 comments: