Anaandika Dixon Busagaga aliyeshiriki zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro.
WAZALENDO 33 kati ya 52 waliojitosa kupandisha bendera ya taifa katika mlima Kilimanjaro kuadhimisha sherehe za Uhuru, wamefanikiwa kufika kilele cha Uhuru na kuacha ujumbe maalumu wa amani.
Waliopeleka bendera hiyo, wamo maofisa wa ngazi ya juu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, makamanda wastaafu wa JWTZ, Wanahabari, watumishi wa Taasisi ya Mkapa Foundation, Shirika la Hifadhi a Taifa (Tanapa) na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro na Jumuiya ya Ushirikiano kati ya Tanzania na China.
Maofisa wa JWTZ waliofika kilele cha mlima Kilimanjaro yumo Luteni Jenerali Mstaafu, James Mwakibolwa ambaye aliwahi kuwa Mnadhimu wa jeshi hilo na Brigedia Jenerali Juma Mwinula.
Kilele cha cha Uhuru chenye urefu wa mita 5,895 ambacho hufunikwa na theluji karibu muda wote ndio kivutio mikubwa kwa watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kundi hilo la wazalendo lilikuwa likiongozwa na Luteni Jenerali Mstaafu James Mwakibolwa ambaye baada ya kurejea , amesema watu 19 wameshindwa kufika kileleni lakini haikuwa uvivu ila sababu za kiafya ambazo wahifadhi walishauri washuke.
"Kikundi hiki kilionyesha moyo wa mshikamano sana, kwa niaba ya wazalendo kwa mshikamano wao.Nawashukuru waongozaji waliokuwa wakituongoza kupanda mlima huo akiwamo Chombo. Walitupeleka pole pole na wala hatukuona magonjwa ya mlima,"alisema Mwakibolwa
Alitaka kuanzia sasa serikali za vijiji zihamasishwe kuwasukuma wananchi kujitokeza kupanda mlima Kilimanjaro kwa kuwa umri siyo tatizo, tatizo ni mawazo tu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Jenerali Mstaafu George Waitara alisema anafurahishwa na damira na ujasiri wa wazalendo hao.
"Nilimkabidhi bendera ya taifa Luteni Jenerali Mstaafu Mwakibolwa pale Mandara na nikamwambia asaidiane na Brigedia Jenerali Mwinula kukipeleka kikundi hiki, nashukuru wote wamefika kilele cha Uhuru," alisema Waitara.
Kutokana na kazi ngumu waliyoifanya wapagazi kuwasaidia wazalendo hao kufika kilele cha Uhuru, Jenerali Mstaafu Waitara amewapa zawadi ya Sh.milioni 3.3 kama asante kwa niaba ya wazalendo 52.
Toa Maoni Yako:
0 comments: