Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Kenya Nchini Tanzania Mhe.Dan Kazungu alipofika kujitambulisha leo Ikulu Mjini Zanzibar akifuatana na ujumbe wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Kenya Nchini Tanzania Mhe.Dan Kazungu alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kujitambilisha akiwa na ujumbe wake (hawapo pichani).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifuatana na Balozi wa Jamhuri ya Kenya Nchini Tanzania Mhe.Dan Kazungu baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar leo alipofika kujitambulisha akifuatana na ujumbe wake (hawapo pichani).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Kenya Nchini Tanzania Mhe.Dan Kazungu baada ya mazungumzo yao alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kujitambulisha. Picha na Ikulu, Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Kenya na Zanzibar zinauhusiano wa kihistoria hivyo ushirikiano katika sekta ya biashara kati ya pande mbili hizo utakuza uchumi na kuuendeleza udugu wa damu uliopo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa Kenya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dan Kazungu aliyefika Ikulu kwa
ajili ya kujitambulisha.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Kazungu kuwa Zanzibar na Kenya zina uhusiano na ushirikiano wa kihistoria hasa katika sekta ya biashara ambapo Zanzibar ilikuwa ndio kitovu kikuu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki tokea karne ya 19.
Dk. Shein alieleza kuwa kuna kila sababu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Kenya katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ambapo kwa upande wa sekta ya biashara ndio sekta pekee yenye historia kati ya pande mbili hizo. Alisema kuwa wananchi wa Kenya na Zanzibar wana udugu wa damu na kutokana na matukio
kadhaa ya kihistoria yakiwemo Watawala waliozitawala nchi hizo yamejenga ukaribu mkubwa na kumpelekea Dk. Shein kusisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein aliunga mkono wazo la Balozi huyo wa Kenya la kuwekwa utaratibu maalum wa kuzidisha ushirikiano huo katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya biashara kati ya Kenya na Zanzibar kwa lengo la kukuza uchumi na kuinua ustawi wa maisha ya wananchi wa pande mbili hizo.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Kenya kwa kununua karafuu za Zanzibar hivi sasa hatua ambayo imesaidia katika kupambana na vita ya biashara ya magendo ya karafuu
iliyokuwa ikiendeshwa na wabadhirifu wa uchumi hapo siku za nyuma.
Akizungumza kuhusu sekta ya utalii, Rais Dk. Shein alisema kuwa kuna haja pia, ya kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Kenya katika kuendeleza sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Kenya imepiga hatua katika sekta ya utalii ikilinganishwa na Zanzibar.
Dk. Shein aliongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa tamaduni zilizofanana kati ya Kenya na Zanzibar, ni vyema pia, katika upande huo kukawepo mashirikiano kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma sambamba na kuwepo mashirikiano ya miji ya Unguja na Mombasa.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa ushirikiano katika sekta ya uvuvi kati ya Kenya na Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na kupambana na umasikini hasa ikizingatiwa kuwa pande mbili hizo zimepitiwa na Bahari ya Hindi na Zanzibar
imezungukwa na Bahari hiyo.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi za makusudi katika kuhakikisha sekta ya uvuvi hasa ule wa kisasa ukiwemo wa bahari kuu inaimarika kwa lengo la kukuza kipato cha wavuvi na kuimarisha uchumi wa Zanzibar kupitia sekta hiyo.
Nae Balozi wa Kenya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dan Kazungu alimpa Rais Dk. Shein salamu za Rais wa Kenya Uhuru Kenyata na kumueleza azma ya kiongozi huyo kukuza uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo kati ya Zanzibar na Kenya.
Balozi Kazungu alimueleza Rais Dk. Shein hamu na nia ya Kenya kukuza uhusiano na ushirikiano na Zanzibar katika sekta ya biashara kwa kutambua sifa na historia kubwa iliyonayo Zanzibar katika sekta hiyo.
Kiongozi huyo, alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Kenya ina mambo mengi ya kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya biashara na iko tayari kuanzisha taratibu zitakazosaidia zaidi kuwepo kwa ushirikiano huo hasa ikizingatiwa kuwa lengo la viongozi wote wa Afrika ni kushirikiana katika kuendeleza mataifa yao na watu wake.
Balozi Kazungu alieleza kuwa mbali ya kuwepo kwa ushirikiano katika sekta ya biashara pia, ipo haja ya ushirikino katika sekta ya uvuvi ambapo katika kuipa kipaumbele sekta hiyo, Balozi huyo alisema kuwa Kenya kwa kushirikiana na Canada hivi karibuni imeandaa mkutano nchini Kenya utakaozungumzia juu ya uchumi wa Bahari “Blue economy” ambapo alisisitiza kuwa ushiriki wa Zanzibar katika mkutano huo una umuhimu mkubwa.
Aliongeza kuwa katika mkutano huo miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na
kuangalia rasilimali za bahari zinatumika vipi katika kusaida kukuza uchumi. Pamoja na hayo, Balozi huyo alisisitiza kuwa ushirikiano katika sekta ya utalii una umhimu mkubwa kati ya Kenya na Zanzibar hasa ikizingatiwa kila uchao Zanzibar imekuwa ikiimarisha miundombinu yake ya kiuchumi ili kukuza sekta ya utalii ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume.
Aidha, alieleza kuwa kutokana na sifa nyingi za kitalii zilizopo Zanzibar watalii wengi
wanaokwenda Kenya wakiwemo wale wanaofika miji mbali mbali ya Kenya ukiwemo mji wa Malindi uliopo Kenya huwa na hamu ya kuja kuitembelea na Zanzibar. Sambamba na hayo, Balozi huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Timu ya Taifa ya Zanzibar “Zanzibar Heroes” kwa kandanda safi iliyoonesha katika fainali ya ubingwa wa Vyama vya
Soka Afrika Mashariki na Kati “CECAFA”, kati ya timu hiyo na timu ya Taifa ya Kenya ambapo
kwa maelezo ya Balozi huyo timu ya Kenya ilipata ushindi kwa tabu pamoja na kujawa na hofu kubwa kutokana na kandanda safi lililooneshwa na vijana wa ‘Zanzibar Heroes’. Balozi huyo pia, aliipongeza Zanzibar kwa kuendelea kuhifadhi na kulinda mazingira ya Zanzibar na kutoa zawadi ya picha aliyomkabidhi Rais Dk. Shein ya marehemu Profesa Wangari Maathai wa Kenya ambaye alipata tunzo ya amani ya Nobel mwaka 2014 kufuatia juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.
Toa Maoni Yako:
0 comments: