Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb) akimkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba kwa kuimarisha sekta ya ushirika nchini wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye dhifa iliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza, Leo 7 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK).
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akitoa salamu za Wizara ya Kilimo kwa Waziri Mkuu wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye dhifa iliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza, Leo 7 Julai 2018.
Baadhi ya wananchi wakifatilia Mkutano wa kilele cha siku ya Ushirika Duniani
Wazori Mkuu Mhe Kassim M. majaliwa akisalimiana na Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege Mkoani Mwanza kwa ajili ya kushiriki sherehe kilele cha siku ya ushirika Duniani kwenye dhifa iliyofanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza, Leo 7 Julai 2018.
Na Mathias Canal-WK, Mwanza.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim M. Majaliwa (Mb) amemkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba kwa kazi kubwa aliyoifanya na anayoendelea kuifanya katika kuimarisha sekta ya ushirika nchini katika kipindi cha muda mfupi tangu alipoteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo.
Tuzo hiyo imetolewa Leo 7 Julai 2018 wakati wa kilele cha siku ya ushirika Duniani na Mhe. Waziri Mkuu kwa niaba ya wanaushirika ambao ndio wameandaa Tuzo hizo ikiwa ni heshima na Utumishi mkubwa kwa Waziri Tizeba katika kipindi kifupi kwa kurudisha imani ya ushirika kwa wananchi waliokuwa wamepoteza matumaini kutokana na baadhi ya viongozi wabadhilifu kujinufaisha na Ushirika kinyume na utaratibu.
Tuzo hiyo kwa Dkt Tizeba inatolewa wakati ambapo ni siku moja pekee imepita tangu Waziri huyo wa kilimo kutangaza Kiama kwa viongozi na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika wanaofanya ubadhilifu wa Mali za wanaushirika kwa manufaa yao pekee pasina kuwanufaisha wanachama wote.
Kwa msisitizo mkubwa hapo jana Julai 6, 2018 Mhe. Dkt Tizeba alieleza kwa ukali kuhusu ubadhilifu wa rasilimali za ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kwenye hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania linalofanyika kwa siku mbili katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.
Kongamano hilo liliambatana na maonesho ya bidhaa na shughuli zinazofanywa na vyama hivyo vya ushirika kote nchini ambapo wanachama wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu, na kujadili mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa sekta ya ushirika nchini na kutoa maoni yao kwa serikali.
Dkt Tizeba amesisitiza kuwa serikali inafanya juhudi mahususi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa dhana kuwa vyama vya ushirika ni kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya biashara ya nchi za nje.
Pia, alisema kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa ushirika wa Taifa katika kuyafikia malengo ya milenia na malengo mbalimbali ya nchi kama uimarishwaji wa sekta ya viwanda, Kilimo, Mifugo, uvuvi na biashara na kuchangia katika ongezeko la kipato kwa wananchi na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
Tuzo hiyo ya kuimarisha sekta ya ushirika nchini pia imetolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli sambamba na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb).
Toa Maoni Yako:
0 comments: