
Na Beda Msimbe, TBN – Moscow, Urusi
Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, amesema nchi yake itaendelea kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano kwa Tanzania ili kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
Rais Putin alitoa kauli hiyo jijini Moscow baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko nchini humo kwa ziara ya kiserikali ya kihistoria.
Amesema Urusi imekuwa ikifuatilia kwa karibu mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayotekelezwa Tanzania na kuridhishwa na hatua kubwa za maendeleo zinazopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.
“Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu maendeleo ya Tanzania na tunafurahishwa na mageuzi yanayofanyika katika sekta mbalimbali za uchumi na ustawi wa jamii. Tunaamini ushirikiano wetu utaendelea kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa nchi zetu,” alisema Putin.
Aliongeza kuwa mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa na tija kubwa na yamefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya biashara, uwekezaji, elimu, teknolojia, nishati na maendeleo ya rasilimali watu.
Putin amesema Urusi itatumia pia Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaotarajiwa kufanyika nchini humo kutangaza na kuhamasisha fursa mbalimbali za uwekezaji zinazoweza kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, kwa sasa Urusi ina miradi takribani 70 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22, ambayo imechangia kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 3,000.
Kwa upande wake, Rais Samia amesema ziara yake nchini Urusi ni ya kihistoria kwa Tanzania kutokana na ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Tanzania kufanya ziara ya kiserikali nchini humo baada ya zaidi ya nusu karne.
“Ziara yangu ina umuhimu wa pekee wa kihistoria kwangu binafsi na kwa nchi yangu. Imepita zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi. Hivyo, kwangu hii ni safari ya kihistoria sana kuja Urusi kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wetu,” alisema Rais Samia.
Rais Samia pia alimshukuru Rais Putin na Serikali ya Urusi kwa mwaliko pamoja na mapokezi na ukarimu aliopatiwa tangu kuwasili kwake nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alikumbusha mchango wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kujenga taifa, huku akimpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya Ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei 9 mwaka huu.
Ziara hiyo ya Rais Samia nchini Urusi ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Tanzania katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, jambo ambalo linaipa uzito mkubwa wa kidiplomasia katika historia ya mahusiano ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao walieleza kuwa mazungumzo yao yamelenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki uliodumu kwa miongo mingi pamoja na kujadili masuala muhimu ya kikanda na kimataifa yanayoendelea duniani.
Ziara ya Rais Samia inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta za uwekezaji, biashara, elimu, sayansi na teknolojia, huku ikichochea fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.





Toa Maoni Yako:
0 comments: