
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatarajia kutoa vibali vya ajira mpya katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa sekta ya afya pamoja na kada nyingine, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza uhaba wa madaktari na wauguzi nchini.
Akizungumza Mei 12, 2026 katika Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Wauguzi lililoambatana na Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika katika Hotel Verde Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika kuboresha huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na ya kisasa.
Alieleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya ikiwemo ujenzi wa Hospitali Mpya ya Mnazi Mmoja pamoja na Hospitali ya Saratani Binguni, sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na kuimarisha mafunzo kwa watumishi wa sekta hiyo.
Rais Dkt. Mwinyi pia aliwataka wauguzi nchini kuendelea kufanya kazi kwa kujituma, huruma na kuzingatia maadili ya taaluma yao, akisisitiza kuwa wauguzi wana nafasi kubwa katika kuimarisha huduma za afya na kuokoa maisha ya wananchi.
Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo, “Kuwawezesha Wauguzi ni Kuokoa Maisha” (Empowering Nurses, Saving Lives).


Toa Maoni Yako:
0 comments: