Nairobi, Kenya — Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward: Africa–France Partnership for Innovation and Growth Summit) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya, ambapo viongozi wa nchi za Afrika na Ufaransa wamekutana kujadili mustakabali wa ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa sekta binafsi, taasisi za kimataifa, wadau wa maendeleo na wawekezaji kutoka pande zote mbili, ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu ikiwemo biashara, teknolojia, nishati, afya, kilimo, Akili Unde (AI), uchumi wa buluu pamoja na viwanda. Majadiliano hayo yanalenga kuharakisha maendeleo endelevu na kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana na wanawake barani Afrika.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mkutano huo ni muhimu kwa Afrika na Ufaransa kwa pamoja kutokana na nafasi ya majadiliano yanayolenga kuimarisha manufaa ya pande zote mbili kupitia ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji. Amesema Afrika ina rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuchochea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Ameongeza kuwa lengo kuu la ushirikiano huo ni kupambana na umasikini na kuongeza ajira kwa makundi mbalimbali, hususan vijana na wanawake ambao ndio nguvukazi kubwa ya bara la Afrika. Aidha, Dkt. Mwigulu amesema maeneo mengi yaliyojadiliwa katika mkutano huo yanalingana moja kwa moja na vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, jambo linaloonesha muunganiko wa ajenda za kikanda na kitaifa katika kukuza uchumi.


Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Samoei Ruto, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha mifumo ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali za ndani, kuongeza uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Amesema ni wakati wa Afrika kubadilika na kujiona kama mdau muhimu katika uchumi wa dunia badala ya kuwa mtazamaji au mnufaika wa misaada pekee.

Rais Ruto amesema Afrika inapaswa kuwa na sauti yenye nguvu katika maamuzi ya kimataifa ya kiuchumi, akisisitiza kuwa baadhi ya mifumo ya sasa ya dunia haijazingatia usawa wa ushiriki wa mataifa ya Afrika. Amesema mshikamano wa Afrika ndio utakaowezesha bara hilo kufikia maendeleo ya muda mrefu na yenye tija.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema Afrika ni bara lenye fursa kubwa na linaloendelea kwa kasi katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kiteknolojia. Amesema Afrika si bara linalosubiri majibu ya changamoto bali ni sehemu inayotoa suluhisho la changamoto zake kupitia ubunifu na uwekezaji.



Katika hotuba yake, Rais Macron ametangaza mpango wa uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 27 barani Afrika, utakaolenga sekta za nishati, Akili Unde (AI), kilimo na uchumi wa bahari. Amesema uwekezaji huo unatarajiwa kuchochea uanzishwaji wa ajira takribani 250,000 barani Afrika na nchini Ufaransa, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande hizo mbili.

Aidha, Rais Macron amewataka wafanyabiashara wa Afrika kutumia fursa zilizopo nchini Ufaransa kuwekeza, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kweli unapaswa kuwa wa pande mbili. Amesema “ushirikiano wa kisasa hauwezi kuwa wa upande mmoja bali ni wa kushirikiana na kunufaika kwa pamoja.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wa Afrika ndio wanakuwa wa kwanza kunufaika na rasilimali za bara lao. Amesema Afrika imejaliwa utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo zikitumika ipasavyo zinaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Mkutano huo unatarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa ukiwa na mijadala mbalimbali ya kimkakati kuhusu uwekezaji, teknolojia, nishati safi, ubunifu na maendeleo ya binadamu, huku ukilenga kuweka msingi mpya wa ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa kwa mustakabali wa maendeleo endelevu. 

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: