Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa na Waziri wa
Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (kushoto), pamoja na Mhe. Prof.
Kitila Alexander Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na
Uwekezaji, wakiwa washiriki wa Programu ya Uongozi wa Mawaziri ya Chuo
Kikuu cha Harvard (Harvard Ministerial Leadership Program). Wapo pia na
mwanafunzi wa Kitanzania wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Bi. Ngasuma Eva
Kanyeka, mshindi wa tuzo inayotolewa na programu hiyo na kudhaminiwa na
taasisi ya Tessa Jowell Foundation. Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa na mwanafunzi wa Kitanzania wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Bi. Ngasuma Eva Kanyeka, mshindi wa tuzo ya Programu ya Uongozi wa Mawaziri ya Chuo Kikuu cha Harvard (Harvard Ministerial Leadership Program), inayodhaminiwa na taasisi ya Tessa Jowell Foundation, pamoja na maafisa wa taasisi hiyo katika Chuo Kikuu cha Harvard, kilichopo Cambridge, jimbo la Massachusetts, nchini Marekani.
Na Mwandishi Maalumu, Havard
Akiwa katika Chuo Kikuu cha Harvard,
jijini Cambridge, jimbo la Massachusetts, nchini Marekani, Rais
Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amempongeza mwanafunzi
wa Kitanzania wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Bi. Ngasuma Eva Kanyeka, kwa
kushinda tuzo inayotolewa na Programu ya Uongozi wa Mawaziri ya Chuo
Kikuu cha Harvard (Harvard Ministerial Leadership Program – HMLP),
inayodhaminiwa na taasisi ya Tessa Jowell Foundation.
Dkt.
Kikwete ni mmoja wa watoa mada katika programu hiyo ya HMLP,
iliyoanzishwa mwaka 2012 kama ushirikiano wa Harvard T.H. Chan School of
Public Health, Harvard Kennedy School of Government na Harvard Graduate
School of Education kwa kushirikiana na Big Win Philanthropy.
Programu
hiyo hufanya kazi na viongozi wa serikali, hususan barani Afrika pamoja
na Asia ya Kusini-Mashariki na Amerika ya Kusini, kwa kuwajengea uwezo
mawaziri kuwa na dira iliyo wazi na uongozi thabiti wa kuendesha mageuzi
makubwa yenye matokeo ya kudumu. HMLP huendesha makundi mawili kila
mwaka, yakijumuisha mawaziri wa sekta mbalimbali pamoja na viongozi wa
ngazi ya juu wenye majukumu ya kitaifa.
Tuzo hiyo yenye
ushindani mkubwa hutolewa kila mwaka kwa mwanafunzi mmoja wa PhD wa
Harvard anayefanya utafiti unaochangia maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Tuzo hiyo inatolewa kwa udhamini wa Tessa Jowell Foundation, taasisi
iliyoanzishwa kuenzi mchango wa marehemu Baroness Tessa Jowell,
aliyekuwa kinara wa kuhimiza mifumo ya afya yenye huruma na maendeleo
jumuishi ya utotoni.
Kwa sasa, taasisi hiyo inaongoza juhudi za
kimkakati katika kuboresha matibabu na huduma za saratani ya ubongo,
pamoja na kuimarisha maendeleo ya awali ya mtoto. Kupitia uchangishaji
fedha, ushawishi wa sera na ushirikiano mpana, inaunganisha wadau kutoka
NHS, serikali, vyuo vikuu na asasi za kiraia ili kuleta mageuzi
endelevu katika sekta ya afya na ustawi wa watoto.
Utafiti wa
Bi. Kanyeka unatumia teknolojia ya akili mnemba (Artificial
Intelligence) kuboresha mifumo ya dhamana ya mikopo (AI credit models),
kwa lengo la kuwawezesha wanawake na vijana kupata mikopo nafuu,
kuongeza kipato na kuboresha afya ya kaya.
Bi. Kanyeka ni
miongoni mwa wanafunzi wachache wa Kitanzania waliopata nafasi ya
kusomea Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Harvard tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1636, na ndiye wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya
kifahari.
Rais Mstaafu Dkt. Kikwete alimpongeza kwa kuiwakilisha
vyema Tanzania katika jukwaa la kimataifa na kuitangaza nchi kwa
heshima kubwa ndani ya Chuo Kikuu cha Harvard.




Toa Maoni Yako:
0 comments: