Na Mwandishi Wetu, Simanjiro.

Wanawake wa Mkoa wa Manyara wameendelea kuimarika kiuchumi baada ya kunufaika na mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh4.2 bilioni iliyotolewa katika kipindi cha miaka miwili ya fedha ya 2024/2025 na 2025/2026, hatua inayotajwa kuwa chachu ya maendeleo ya familia na jamii.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Kijiji cha Orkirung’rung’, Kata ya Endonyongijape, Wilaya ya Simanjiro, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga, alisema uwezeshaji huo wa kiuchumi kwa wanawake unaendana na juhudi za serikali za kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 wanawake wa mkoa huo walipokea mikopo yenye thamani ya Sh3 bilioni, huku mwaka wa fedha wa 2025/2026 hadi kufikia mwezi Februari tayari kiasi cha Sh1.2 bilioni kikiwa kimeshatolewa.

RC Sendiga alisema mafanikio hayo yanaonyesha jinsi wanawake wa Manyara wanavyojituma katika kujiletea maendeleo na kuchangia ustawi wa uchumi wa mkoa huo.

“Hongereni sana wanawake wa Manyara kwa juhudi zenu. Kupitia kauli mbiu ya Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050, tunaamini wanawake wataendelea kuwa injini muhimu ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Sendiga.

Katika hotuba yake, RC Sendiga aliwataka wazazi na jamii kwa ujumla kulinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo, akitaja vitendo vya vipigo, unyanyasaji na ukeketaji kuwa ni changamoto zinazopaswa kupingwa kwa nguvu zote.

Alisema jamii inapaswa kuachana na mila na desturi kandamizi zinazodhalilisha haki za wanawake na wasichana.

“Yawezekana miongoni mwetu tumekua tumeshuhudia au hata kukumbana na ukeketaji, jambo ambalo halikuwa sahihi. Ndiyo maana sasa dunia inapiga kelele kupinga vitendo hivi. Tuwalinde watoto wetu dhidi ya ukeketaji na aina zote za ukatili wa kijinsia,” alisema.

RC Sendiga aliongeza kuwa wanawake wanapaswa kung’ara katika nyanja mbalimbali za maisha ikiwemo uchumi, ujasiriamali, elimu, uongozi na malezi bora ya watoto ili kujenga jamii imara yenye ustawi.

Alisisitiza kuwa mwanamke ana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko katika familia na jamii bila kusubiri kushika nafasi za uongozi.

“Mwanamke ana uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya familia na jamii. Tunapaswa kuhakikisha tunasimama imara kupambana na ukatili wa kijinsia na wakati huo huo kujenga uchumi wa familia kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo,” alisema.

Aidha, RC Sendiga aliwahamasisha wanawake na wananchi wa Manyara kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisema mpango huo utasaidia familia nyingi kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu.

Alieleza kuwa kwa gharama ya takribani Sh150,000 kwa mwaka, familia ya watu sita — baba, mama na watoto wanne — inaweza kupata huduma za matibabu, jambo ambalo litasaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi.

“Ninaamini wananchi wengi watajitokeza kujiandikisha kwenye mpango huu ili waweze kupata kadi za matibabu na kuhakikisha familia zao zinakuwa salama kiafya,” alisema.

Awali akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa mkoa huo, Belinda Sumari alisema pamoja na juhudi za serikali kuwawezesha wanawake kiuchumi, bado kuna changamoto kadhaa zinazoathiri maendeleo yao ikiwemo ukosefu wa mitaji ya kutosha kwa ajili ya ujasiriamali.

Alisema pia changamoto za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo ukeketaji na ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi za uongozi, bado zinaathiri ushiriki wao katika maamuzi muhimu ya maendeleo.

“Wanawake wa Manyara tunaendelea kupambana kuhakikisha ndoto zetu na za watoto wetu hazizimwi na changamoto, kwani tunaamini kila changamoto ni daraja la kufikia mafanikio makubwa,” alisema.

Katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa maendeleo kutoka halmashauri zote saba za mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala, alimkabidhi RC Sendiga tuzo maalum ya kutambua uongozi wake thabiti na mchango wake katika kuleta maendeleo, amani na utulivu mkoani Manyara.

Vilevile, baadhi ya wadau wa maendeleo akiwemo Taiko Kulunju na Mula Sanare Lesiangiki walitunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao katika kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoani humo.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: