Na Mwandishi Wetu.
Dodoma — Serikali imetangaza rasmi kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Vangimembe Lukuvi, kilichotokea leo Machi 25, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa kwa umma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kiongozi huyo amefariki dunia majira ya saa moja asubuhi akiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu kufuatia ugonjwa wa mshtuko wa moyo.
Katika taarifa hiyo, Rais Samia ameeleza kusikitishwa na msiba huo mzito, akitoa pole kwa Spika wa Bunge, familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Isimani pamoja na Watanzania wote kwa ujumla.
“Kifo cha Mheshimiwa Lukuvi ni pigo kubwa kwa Taifa, kutokana na mchango wake mkubwa katika uongozi na utumishi wa umma,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Marehemu Lukuvi alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikalini kwa muda mrefu, akitambulika kwa uzalendo wake na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Serikali imesema itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi kadri zitakavyopangwa.



Toa Maoni Yako:
0 comments: