
Kupitia uteuzi huo, Dk. Songwe anaungana na kundi la wasomi mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya tafiti na kutoa ushauri kwa Kanisa kuhusu changamoto za maendeleo ya dunia, haki za kijamii na ustawi wa jamii.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Songwe aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika mfumo wa United Nations, ikiwemo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo na Katibu Mtendaji wa United Nations Economic Commission for Africa. Katika nafasi hizo, alihusika katika kuandaa sera na mikakati ya kuimarisha maendeleo ya uchumi barani Afrika.
Taasisi ya Pontifical Academy of Social Sciences ilianzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kukusanya wataalamu wa kimataifa kutoka fani mbalimbali kama uchumi, sosholojia, sheria na sayansi ya siasa ili kusaidia Kanisa Katoliki kuelewa na kutoa mwongozo kuhusu changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoikabili dunia.
Ingawa wanawake hawaruhusiwi kuwa mapadre au maaskofu ndani ya Kanisa Katoliki, katika miaka ya karibuni Vatican imeanza kuwateua wanawake wachache katika nafasi za juu za ushauri na uongozi.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya Kanisa, uteuzi wa Dk. Songwe ni hatua muhimu katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika taasisi za juu za Kanisa Katoliki duniani. Kutoka barani Afrika, anatajwa kuwa mwanamke wa tatu kuwahi kuteuliwa katika nafasi hiyo na Papa.
Hatua hiyo pia inaonekana kuimarisha mchango wa wasomi wa Afrika katika majadiliano ya kimataifa kuhusu maendeleo ya kijamii na kiuchumi duniani.


Toa Maoni Yako:
0 comments: