Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imetupilia mbali shauri la mapitio lililofunguliwa kupinga uundwaji wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.

Shauri hilo la Mapitio Namba 32537 la mwaka 2025 lilifunguliwa na Rosemary Mwakitwange pamoja na wenzake watatu dhidi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wajumbe wa Tume hiyo ya Uchunguzi.

Katika maombi yao, walalamikaji waliiomba Mahakama Kuu ya Tanzania itoe amri ya kufuta uamuzi wa Samia Suluhu Hassan wa kuunda na kuteua wajumbe wa Tume hiyo tarehe 18 Novemba 2025, wakidai kuwa Rais alivuka mipaka ya mamlaka yake ya kisheria wakati wa kuunda chombo hicho.

Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama Kuu tarehe 13 Machi 2026 ilitupilia mbali shauri hilo, ikieleza kuwa Rais alitumia mamlaka yake kwa mujibu wa sheria wakati wa kuunda Tume hiyo.

Katika uamuzi wake, Mahakama ilieleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, kifungu cha 3 kinampa Rais mamlaka ya kuunda Tume ya Uchunguzi na kuteua wajumbe wake.

Mahakama ilibainisha pia kuwa hakuna ushahidi uliowasilishwa unaoonesha kuwa Rais alivunja sheria au kwenda kinyume na matakwa ya sheria hiyo wakati wa kuunda Tume hiyo.

Aidha, Mahakama haikuona dalili ya upendeleo katika uteuzi wa wajumbe wa Tume, ikisisitiza kuwa sheria inampa Rais mamlaka ya kufanya uteuzi huo bila kuwekewa masharti ya ziada.

Kutokana na hoja hizo, Mahakama ilihitimisha kuwa maombi ya walalamikaji hayakuwa na msingi wa kisheria, hivyo ikaamua kuyatupilia mbali.

Shauri hilo liliendeshwa na jopo la mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, waliowakilisha Serikali katika shauri hilo.

Uamuzi huo unathibitisha uhalali wa kisheria wa uamuzi wa Rais wa kuunda Tume ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa kutokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 nchini.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: