
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, marehemu Bungara alifariki dunia wakati akiwa hospitali alipokwenda kupata huduma ya kusafisha figo (dialysis).
Chama hicho kimetoa pole za dhati kwa familia ya marehemu, hususan kwa mjane wake Bi. Mwanawetu Said Zarafi, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo mzito.
ACT Wazalendo imemkumbuka marehemu Bungara kama mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa jasiri na aliyejitolea kupigania haki, demokrasia na ustawi wa wananchi katika maisha yake yote.
Aidha, chama hicho kimeeleza kushiriki kikamilifu katika msiba huo kwa kuchangia hali na mali, ikiwemo kugharamia mazishi ya marehemu. Pia kimewaomba wanachama wake, hususan kutoka Kanda ya Kilwa Kusini, kujitokeza kwa wingi kushirikiana na familia katika kipindi hiki kigumu.
“Tunaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki cha majonzi, na tunaomba Mwenyezi Mungu aipokee roho ya marehemu mahali pema peponi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kifo cha Bungara kimeacha pengo kubwa ndani ya chama hicho na kwa wanasiasa wa upinzani nchini, huku akitarajiwa kukumbukwa kwa mchango wake katika harakati za kisiasa na kijamii.


Toa Maoni Yako:
0 comments: