RUVUMA, Februari 28, 2026 — Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo, ametoa wito kwa Watanzania kugeuza historia ya mashujaa wa Vita vya Maji Maji kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi badala ya kubaki katika kumbukumbu pekee.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa wa Vita vya Maji Maji yaliyofanyika mkoani Ruvuma, Mwalongo alisema mashujaa hao walionesha ujasiri, umoja na uzalendo wa hali ya juu katika kupigania ardhi, heshima na utu wa Mwafrika, jambo linalopaswa kuwa dira ya kizazi cha sasa.

Alisema damu ya mashujaa hao ndiyo iliyopanda mbegu ya uhuru wa taifa, hivyo ni wajibu wa Watanzania kuhakikisha historia hiyo inatumika kujenga uchumi, maarifa na mshikamano wa kijamii.
Mwalongo alisisitiza kuwa maadhimisho hayo yanapaswa kuwa jukwaa la kuhamasisha uwekezaji katika utalii wa kihistoria, tafiti za kisayansi pamoja na matumizi ya teknolojia katika kuhifadhi makumbusho na nyaraka muhimu za historia. Aliongeza kuwa maeneo ya kihistoria yanaweza kuboreshwa na kuwa vivutio vya utalii, hatua itakayosaidia kufungua ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa maeneo husika.

Aidha, aliwataka wadau mbalimbali kushirikiana katika kuhifadhi mazingira pamoja na kuendeleza tiba asili kama sehemu ya kulinda urithi wa taifa na maarifa ya jadi.

Maadhimisho hayo yameendelea kuwa sehemu muhimu ya kukumbuka mapambano dhidi ya ukoloni huku yakihamasisha kizazi cha sasa kujivunia historia na utamaduni wao.

“Mashujaa wetu tunawaenzi leo na milele, na njia bora ya kuwaenzi ni kujenga taifa lenye maendeleo, mshikamano na heshima kwa urithi wake,” alihitimisha Mwalongo.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: