
Na Mwandishi Wetu
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu, FIFA, limethibitisha rasmi ushiriki wa Nigeria katika mashindano ya FIFAe Nations League 2026, hatua inayotajwa kuimarisha nafasi ya taifa hilo katika ulimwengu wa michezo ya kielektroniki (esports).
Kwa mujibu wa taarifa ya FIFA, mashindano ya msimu ujao yatahusisha mikondo mitatu ambayo ni eFootball ya console, eFootball ya simu, pamoja na Rocket League. Takwimu zinaonesha kuwa jumla ya nchi 115 zimefuzu katika kundi la console, 81 katika mobile na 84 katika Rocket League, huku Nigeria ikifanikiwa kufuzu katika makundi yote matatu.
Ushiriki huo unalipa taifa hilo fursa mpya ya kujipambanua kimataifa baada ya kushindwa kufika mbali katika Kombe la Dunia la FIFAe 2025 lililofanyika Saudi Arabia, ambapo timu ya Nigeria ilitolewa hatua ya robo fainali baada ya kufungwa na Afrika Kusini.
Wakati huohuo, macho ya wadau wa soka bado yanaelekezwa kwa uamuzi unaotarajiwa kutolewa na FIFA kuhusu rufaa iliyowasilishwa na Nigeria Football Federation dhidi ya Fédération Congolaise de Football Association kuhusiana na madai ya uhalali wa mchezaji katika mchezo wa mtoano wa kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Katika mchezo huo, DR Congo ilisonga mbele kwa ushindi wa mikwaju ya penalti na kufuzu hatua ya mtoano wa kimataifa, lakini iwapo FIFA itaamua kuipatia haki Nigeria, timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles, inaweza kurejeshwa katika hatua hiyo.
Hata hivyo, kwa sasa uthibitisho wa ushiriki wa Nigeria katika FIFAe Nations League unaonekana kuwa faraja kubwa na hatua muhimu katika kukuza ndoto za taifa hilo ndani ya sekta inayokua kwa kasi ya esports duniani.


Toa Maoni Yako:
0 comments: