Na Mwandishi Wetu, Geita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Karia Magaro, amesisitiza umuhimu wa uongozi unaozingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa Halmashauri ili kuhakikisha maamuzi yanayofikiwa yanazingatia hekima, busara na maslahi mapana ya wananchi. Kauli hiyo aliitoa wakati wa kuhitimisha hotuba yake katika Mkutano wa Kawaida wa Robo ya Pili wa Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika mkutano huo, Magaro alieleza kuwa utekelezaji wa bajeti iliyopitishwa unahitaji ufuatiliaji wa karibu na mshikamano baina ya viongozi wa kuchaguliwa na watumishi wa Halmashauri, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu ya kulinda utulivu na kuongeza ufanisi wa utendaji wa taasisi hiyo.

Akitoa taarifa ya mapato na matumizi, Magaro alisema Halmashauri imefanikiwa kukusanya Shilingi bilioni 6.3 za mapato ya ndani, sawa na asilimia 45.42 ya lengo la mwaka. Aidha, Halmashauri imepanga kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 20.9, fedha zitakazotokana na mapato ya ndani, wahisani pamoja na Serikali Kuu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Silvester Kahesi, alipongeza ushirikiano uliopo kati ya madiwani na wataalamu kuanzia ngazi ya kamati hadi Baraza, akieleza kuwa mshikamano huo umechangia kufanikisha vikao vyenye tija na maamuzi yanayoakisi matarajio ya wananchi wa Geita.

Katika hatua nyingine, Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Geita lilielekezwa kuongeza juhudi katika kusimamia na kuboresha hali ya usafi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro. Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Katibu Tawala wa Wilaya, Lucy Beda, alisema kuwa Katoro ni lango muhimu la mkoa na ni lazima hadhi yake iendane na usafi wa mazingira, hususan ikizingatiwa kuwa ni eneo linalopokea viongozi na wageni mbalimbali wanaoingia mkoani Geita.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: