Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza mchakato wa kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya mchango wa sekta ya sanaa na burudani katika Pato la Taifa, kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga sera na maamuzi ya maendeleo ya sekta hiyo.
Hatua hiyo imebainishwa Februari 04, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini, kilichowakutanisha wadau mbalimbali akiwemo Mwakilishi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Mawazo Kibamba, pamoja na wataalamu kutoka taasisi za umma.
Akifungua kikao kazi hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara hiyo, Bw. Benard Lubogo, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu ili waweze kufanya ukokotoaji sahihi wa mchango wa sekta ya sanaa na burudani katika uchumi wa Taifa.Bw. Lubogo alieleza kuwa sekta ya sanaa na burudani imekuwa ikikua kwa kasi na kutoa ajira kwa wananchi wengi, hivyo ni muhimu kuwa na takwimu zinazoonesha mchango wake halisi katika Pato la Taifa ili iweze kupewa uzito unaostahili katika mipango ya kitaifa.

Kwa upande wake, Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bw. Pastory Ulimali, alisema kuwa sanaa na burudani ni miongoni mwa sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa ajira, jambo linaloongeza idadi ya walipakodi na hatimaye kukuza mapato ya Serikali.
Aliongeza kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi utaisaidia Serikali kutambua mchango wa kweli wa sekta hiyo, kuweka mikakati madhubuti ya kuiendeleza na kuongeza tija kwa wasanii, wafanyabiashara wa burudani pamoja na uchumi wa nchi kwa ujumla.



Toa Maoni Yako:
0 comments: