Na Mwandishi Wetu.

DAR ES SALAAM: Wataalamu wa masuala ya jamii na saikolojia wameeleza kuwa changamoto nyingi zinazohusishwa na mitandao ya kijamii hazisababishwi na teknolojia yenyewe bali ni ukosefu wa nidhamu, kujitawala na uelewa wa watumiaji. 

Kauli hiyo imesisitizwa na mtaalamu wa masuala ya kijamii, Dkt. Chris Nwachukwu, akieleza kuwa mitandao ya kijamii ni kioo kinachoakisi tabia za binadamu.

Akizungumza kupitia makala yake ya kielimu, Dkt. Nwachukwu amesema mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, TikTok na X (zamani Twitter) imeleta mapinduzi makubwa katika mawasiliano, elimu na biashara, lakini matumizi yasiyo na nidhamu yameibua changamoto kama uraibu, maisha ya kuigiza, utegemezi wa misaada ya mtandaoni na njaa ya kuthaminiwa kwa “likes”.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, uraibu wa mitandao ya kijamii unatokana zaidi na kushindwa kujidhibiti kuliko teknolojia yenyewe. Amesema watu wengi hutumia muda mwingi mtandaoni wakikwepa majukumu ya msingi kama kazi, masomo na familia, hali inayochochewa na upweke, msongo wa mawazo na kutokuwepo kwa malengo binafsi.

Ameongeza kuwa mitandao hiyo imekuza utamaduni wa maisha ya kuigiza, ambapo baadhi ya watumiaji huonyesha maisha ya kifahari yasiyo halisi, hali inayosababisha wivu, msongo wa mawazo na hata maamuzi mabaya ya kifedha. “Tatizo si picha au video, tatizo ni kushindwa kuchambua ukweli na kudhibiti hisia,” amesema.

Dkt. Nwachukwu pia amegusia ongezeko la tabia ya kuomba misaada mtandaoni bila mipaka, akisema hali hiyo inachochea utegemezi na kuporomosha uwajibikaji binafsi. Amesisitiza kuwa kusaidia ni jambo jema, lakini bila nidhamu kunazalisha utamaduni wa kuomba badala ya kufanya kazi.

Kuhusu afya ya akili, amesema njaa ya kuthaminiwa kupitia ‘likes’ na ‘followers’ imewafanya baadhi ya watu kupima thamani yao kwa idadi ya maoni mtandaoni, jambo linalodhuru ustawi wa kisaikolojia. “Nidhamu ya ndani ndiyo ngao dhidi ya shinikizo la uthibitisho wa mtandaoni,” ameeleza.

Kwa kuhitimisha, Dkt. Nwachukwu amesema mitandao ya kijamii ikitumika kwa nidhamu inaweza kuwa chombo chenye nguvu cha elimu, ujasiriamali na mabadiliko ya kijamii. Ameitaka jamii, hususan vijana, kujenga maadili, kujitawala na fikra makini ili kuitumia teknolojia kwa maendeleo badala ya kujiharibia maisha.

Amesisitiza kuwa suluhisho si kuilaumu mitandao ya kijamii, bali ni kujenga nidhamu ya matumizi, akisema: “Mitandao ya Jamii si adui; nidhamu ndiyo ufunguo wa mafanikio.”

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: