
Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam — Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetoa taarifa kwa umma ikionya kuhusu matumizi sahihi ya dawa zenye kiambata hai cha levonorgestrel pamoja na dawa ya misoprostol, kufuatia taarifa zinazosambaa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zinazoweza kupotosha watumiaji.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa Januari 22, 2026, TMDA imesema levonorgestrel ni kiambata kinachotumika kwenye baadhi ya dawa za uzazi wa mpango na dawa za dharura za kuzuia mimba baada ya tendo la ndoa (emergency contraceptives). Dawa hizo hutakiwa kutumika ndani ya muda usiozidi saa 72 baada ya kufanya tendo la ndoa bila kinga, na matumizi yake yanapaswa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya.
TMDA imeeleza kuwa baadhi ya taarifa potofu zimekuwa zikidai kuwa dawa hizo zinaweza kutumika kutoa mimba, jambo ambalo si sahihi kitaalamu. Mamlaka imefafanua kuwa levonorgestrel haitumiki kutoa mimba, bali huzuia mimba kutungwa endapo itatumika kwa wakati unaopendekezwa.
Kwa upande wa dawa ya misoprostol, TMDA imeonya kuwa matumizi yake bila ushauri wa mtaalamu wa afya ni hatari kwa afya ya mwanamke. Ingawa kitaalamu misoprostol hutumika katika mazingira maalumu ya kitabibu kama kusaidia wakati wa kujifungua, kuzuia kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua, na katika baadhi ya matibabu ya tumbo, matumizi yake holela yamehusishwa na madhara makubwa kiafya ikiwemo kutokwa damu nyingi, maumivu makali ya tumbo, kichefuchefu, kutapika, kuharisha na hatari kwa maisha.
TMDA imewahimiza wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kabla ya kutumia dawa yoyote, hususan zinazohusiana na afya ya uzazi, na kuepuka kuamini taarifa zisizo rasmi kutoka mitandao ya kijamii au vyanzo visivyo vya kitaalamu.
Aidha, mamlaka hiyo imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya dawa na kuwasisitiza wananchi kutoa taarifa kwa TMDA endapo watakutana na matumizi mabaya ya dawa au taarifa zinazoweza kuhatarisha afya ya jamii.
TMDA imesisitiza kuwa usalama wa afya ya mwananchi ndiyo kipaumbele chake kikuu, na matumizi sahihi ya dawa ni msingi muhimu wa kulinda maisha.


Toa Maoni Yako:
0 comments: