Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Marekani katika matumizi ya teknolojia na vifaa vya kisasa ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za utafiti katika sekta ya madini, hususan madini ya kinywe (graphite).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 21, 2026, Mhe. Mavunde amesema Wizara ya Nishati na Madini ya Serikali ya Marekani itatoa mafunzo kwa wataalamu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kupitia programu maalum ya kujenga uwezo, itakayohusisha mafunzo ya siku mbili yenye lengo la kuwaongezea ujuzi wa kitaalamu katika utafiti wa madini.

Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano huo, Tanzania itaongeza maeneo yaliyofanyiwa utafiti wa kina wa madini na iko tayari kushirikiana na mataifa mbalimbali, ikiwemo Marekani, katika kuendeleza shughuli za utafiti wa rasilimali zake.
Mhe. Mavunde ameongeza kuwa maeneo yatakayofanyiwa utafiti ni pamoja na leseni zinazosimamiwa na STAMICO, ambapo utafiti wa pamoja utafanyika ili kubaini maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini. Hatua hiyo inatarajiwa kuchochea kuanzishwa kwa migodi mikubwa, hususan katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Amebainisha kuwa kufikia mwaka 2050, mahitaji ya madini ya kinywe duniani yanatarajiwa kufikia tani milioni 4.5 kwa mwaka, hali inayoiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa mmoja wa wasambazaji wakuu wa madini hayo katika soko la kimataifa.

Aidha, Waziri Mavunde amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali za madini, jambo linaloifanya Marekani kuanzisha programu ya kusaidia maendeleo ya sekta ya madini nchini, ikizingatiwa pia kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Andrew Lentz, amesema Marekani ina furaha kubwa na kiwango cha ushirikiano kinachotolewa na Tanzania katika utekelezaji wa mradi huo muhimu, unaolenga kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili. Ameongeza kuwa Marekani ina nia ya kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano huo katika siku zijazo.

Ushirikiano huu kati ya Tanzania na Marekani katika utafiti wa madini ya kinywe unatarajiwa kuimarisha sekta ya madini kupitia utafiti wa kina, ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani na kuvutia uwekezaji mkubwa, hatua itakayoiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na ongezeko la mahitaji ya madini hayo duniani.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: