Na Mwandishi Wetu – WMJJWM, Ifakara.

Serikali kupitia Halmashauri ya Mji Ifakara imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 600 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Mikopo hiyo ilitolewa Januari 27, 2026 katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Stendi ya Mabasi Kibaoni, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wanufaika wa mikopo hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felista Mdemu, aliipongeza Halmashauri ya Mji Ifakara kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba.
Mdemu aliwataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa, kuzingatia masharti ya mikataba na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kunufaika na mpango huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya halmashauri, kati ya shilingi milioni 600 zilizotengwa, shilingi 404,787,300 tayari zimekwishatolewa kwa vikundi 41, vikiwemo vikundi 20 vya wanawake, 17 vya vijana na vinne vya watu wenye ulemavu, huku fedha hizo zikiwa tayari zimeingizwa kwenye akaunti za vikundi husika. Kiasi kilichosalia cha shilingi 195,212,700 kinatarajiwa kutolewa kwa vikundi 17 baada ya kukamilisha maboresho yaliyoelekezwa.

Mgawanyo wa mikopo umezingatia makundi maalum ambapo vikundi saba vya wajane vyenye wanufaika 60 vimepatiwa shilingi 42,975,000, huku vikundi viwili vya wanawake wanaoishi na VVU vyenye wanufaika 31 vikipewa shilingi 18,269,000.
Kwa upande wa aina za shughuli, vikundi vya usafirishaji vimepokea jumla ya shilingi 239,400,000 kwa vikundi 18, vikundi vya kilimo vimepatiwa shilingi 82,693,650 kwa vikundi 13, na vikundi vya ufugaji vimepokea shilingi 82,693,650 kwa vikundi 10.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Bi. Pilly Kitwana, amewahimiza wananchi kuendelea kuunda vikundi ili waweze kunufaika na mikopo hiyo, akibainisha kuwa bado fedha zipo kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wengi zaidi.

Kitwana pia ameahidi kuwa halmashauri itaendelea kufanya tathmini na ufuatiliaji wa karibu kwa vikundi vilivyonufaika ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija, inaongeza kipato cha wanufaika na kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa jamii kwa ujumla.

Hatua hii inaonesha dhamira ya Serikali kuendelea kuwainua wananchi kiuchumi na kujenga uchumi shirikishi unaowawezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: