Na Jackline Minja – MJJWM, Dodoma

Serikali imesema haioni haja ya kuweka sharti la kisheria linalowalazimisha watoto kuwahudumia wazazi wao wasiojiweza, ikibainisha kuwa jukumu hilo tayari linashughulikiwa kupitia misingi ya kifamilia na kijamii.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Mhe. Tarimba Gulam Abbas, lililohoji kuhusu uwezekano wa kuwekwa kwa sharti la kisheria la watoto wakubwa kutunza wazazi wao wasiojiweza.

Akijibu swali hilo, Mhe. Mahundi amesema Serikali inatambua umuhimu wa familia na jamii katika kulea na kutunza wazee, akisisitiza kuwa huu ni msingi wa mila na desturi za Kitanzania.

“Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa familia na jamii katika kuchukua jukumu la kulea na kutunza wazee, kwani huu ndio msingi wa mila na desturi za Kitanzania na nguzo muhimu katika kujenga mshikamano wa kijamii,” amesema.

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha huduma na matunzo kwa wazee kupitia Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, ambayo hivi karibuni imepitishwa katika toleo la mwaka 2024. Sera hiyo inaweka bayana wajibu wa familia na jamii katika kusimamia matunzo ya wazazi na wazee kwa ujumla, huku ikisisitiza kuimarisha mifumo ya kisheria itakayolinda na kuendeleza ustawi wa wazee pamoja na watoto wanaowatunza.

“Kwa sasa Serikali ipo katika hatua ya kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kutoa maoni juu ya masuala muhimu ya kuzingatiwa katika sheria hiyo,” amesema Mhe. Mahundi.

Aidha, Naibu Waziri amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha maadili ya uwajibikaji wa kifamilia na kuimarisha mifumo ya kijamii inayosaidia ustawi wa wazee nchini.

Hali hii inaashiria dhana ya Serikali kuwa kulea wazee ni jukumu la kijamii na la kifamilia, badala ya kuwalazimisha watoto kupitia sheria, huku ikiendelea kuboresha huduma za kijamii na kisheria zinazohakikisha ustawi wa wazee nchini.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: