
Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam January 27, 2026: Kadri Watanzania wanavyoendelea kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wadau wa maendeleo wameibuka kueleza namna utawala wake wa miaka mitano ulivyogeuka kuwa nguzo muhimu ya mageuzi ya kijamii na kiuchumi, hususan kwa vijana.
Mratibu wa Taasisi ya Together for Samia, Gulatone Masiga, amesema kuwa kipindi cha uongozi wa Rais Samia kimeweka historia mpya kwa kuwalenga vijana moja kwa moja kupitia sera na mipango inayogusa ajira, elimu, ujuzi na uwezeshaji wa kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Januari 26, 2026, wakati wa maadhimisho yaliyoandaliwa na taasisi hiyo, Masiga amesema Rais Samia amefungua milango ya fursa ambazo hapo awali zilikuwa ndoto kwa vijana wengi.
“Serikali ya awamu ya sita imewekeza kwa vitendo. Ujenzi wa vyuo vya ufundi na ujuzi katika zaidi ya wilaya 62 umebadilisha mwelekeo wa vijana kutoka kusaka ajira kwenda kujiajiri na kushindana katika soko la ajira,” amesema Masiga.
Ameongeza kuwa mageuzi katika sekta ya elimu, hususan kuanzishwa kwa mtaala mpya unaozingatia maarifa na stadi za maisha, umeongeza uwezo wa wanafunzi wanaomaliza shule kuwa wabunifu na kujitegemea kiuchumi.
Kwa upande mwingine, uwekezaji wa serikali katika nishati safi umetajwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa viwanda na biashara ndogo ndogo, hali inayowapa vijana mazingira bora ya kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana Innovations, Dorcas Mshiu, amesema maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais Samia yana maana kubwa kwa vijana kwa kuwa ni kiongozi aliyeleta mabadiliko ya moja kwa moja katika maisha yao.
Mshiu amesema kupitia mazingira bora ya biashara yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita, vijana wengi wamefanikiwa kusajili biashara zao na kupanua wigo wa uwekezaji ndani na nje ya nchi.
“Mpango wa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia nne kwa vijana ni hatua ya kihistoria. Imewasaidia wengi kuanza na kukuza miradi yao,” amesema.
Kwa upande wake, mshiriki wa tukio hilo, Nathaniel Samson, amewataka Watanzania kuendelea kumuombea Rais Samia, akisema ni kiongozi anayesimamia ahadi zake kwa vitendo.
Kauli za wadau hawa zinaonyesha wazi kuwa kwa vijana wengi, uongozi wa Rais Samia haujaishia kwenye sera na maneno, bali umejidhihirisha katika matokeo yanayoonekana katika maisha ya kila siku.




Toa Maoni Yako:
0 comments: